Tanzania U19 yang’ara Kriketi Afrika
TIMU ya taifa ya Tanzania ya Kriketi kwa vijana chini ya umri wa miaka 19 imeanza vyema michuano ya Afrika daraja la pili kufuzu Kombe la Dunia baada ya kuichapa Nigeria kwa mikimbio 128-127.
Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Gymkhana Dar es Salaam,utofauti wa mikimbio ni moja huku Tanzania ikicheza wiketi nne na Nigeria 10.
Nahodha wa timu hiyo Laksh Bakrania amesema mchezo ulikuwa mzuri na mgumu ila juhudi zao zimewasaidia kupambana na kushinda.
Kesho watacheza na Ghana ambao nao wametoka kushinda mchezo dhidi ya Msumbiji kwa mikimbio 81-80.
Michuano hiyo ya Afrika inafanyika kwenye viwanja vya Gymkhana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambapo imeshirikisha nchi nane ambazo ni Tanznia, Nigeria, Malawi , Msumbiji, Ghana, Botswana, Siera Leone na Rwanda.
Tanzania ipo kundi B lenye timu za Nigeria, Msumbiji na Ghana huku kundi A kukiwa na Sierra Leone, Rwanda, Botswana na Malawi.
Mratibu wa mashindano hayo Atif Salum amesema nchi mbili kwa kila kundi zitaenda kucheza nusu fainali na zile zitakazofanya vizuri zitaenda fainali.
“Kutakuwa na mchezo pia wa kutafuta mshindi wa tatu. Timu tatu zitakazofanya vizuri zitafuzu daraja la kwanza,”amesema.
Mwenyekiti wa Chama cha Kriketi Tanzania (TCA) Dk Balakrishna Sreekumar amesema wanataka kuinua mchezo huo na kuhakikisha unakuwa miongoni mwa Michezo maarufu nchini huku akiishukuru serikali kwa kuwa pamoja nao.
Amesema wamealika vijana100 kutoka shule 10 za Dar es Salaam ili kutazama mchezo huo na kuwapa hamasa ya kujiunga.
Michuano hiyo inatarajiwa kuendelea hadi Agosti 11 watakapopatikana washindi watatu watakaofuzu daraja la kwanza na kushiriki fainali za Dunia.