Muziki

Tyla aikana Roc Nation, ajikita kwenye albamu yake

JOHANNESBURG: Mwanamuziki nyota wa Afrika Kusini, Tyla, ameendelea kuwa gumzo duniani baada ya tetesi zilizomuhusisha na kampuni kubwa ya burudani ya Marekani, Roc Nation inayomilikiwa na rapa maarufu Jay-Z.

Taarifa hizo zilisambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii baada ya picha za kidijitali zilizoonesha ujumbe wa kumkaribisha Tyla kwenye familia ya Roc Nation kuanza kusambazwa, jambo lililowafanya mashabiki wengi kuamini kuwa msanii huyo alikuwa ameanza ukurasa mpya wa kazi yake.

Hata hivyo, Tyla mwenyewe alijitokeza kuweka wazi hali halisi, akikanusha taarifa hizo na kusema hajawahi kusaini mkataba na Roc Nation. Badala yake, msanii huyo alielekeza nguvu zake kwenye maandalizi ya albamu yake mpya ‘APOP’.

Licha ya kukanusha taarifa hizo, jina la Tyla limeendelea kuwa moja ya majina makubwa katika muziki wa Afrika kutokana na mafanikio yake ya kimataifa, hususan baada ya wimbo wake ‘Water’ kumpa umaarufu mkubwa duniani na kumuingiza kwenye historia ya wasanii wa Afrika waliopata mafanikio makubwa kwenye jukwaa la kimataifa.

Tukio hilo limeonyesha ukubwa wa ushawishi wa Tyla katika tasnia ya muziki, ambapo hata tetesi za hatua yake ya kibiashara ziliweza kutengeneza mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki na vyombo vya habari duniani.

Related Articles

Back to top button