Nyumbani

Mkwasa afichua sakata la usajili wake Simba walimpa Sh: 45,000, akachagua Yanga

...mashabiki wa Simba waliniita mwizi

DAR ES SALAAM: Nguli wa soka Tanzania, Boniface Mkwasa, amefichua simulizi ya kipekee kuhusu sakata la usajili wake, akieleza jinsi alivyosajiliwa na Yanga licha ya Simba kufika baadaye na kukubali masharti aliyoweka akiamini yasingekubalika.
Mkwasa amesema tayari alikuwa mchezaji wa Yanga kabla Simba hawajaonesha nia ya kumtaka. Alidai alipoulizwa na Simba kiasi alichotaka, alitaja Sh45,000 akiamini fedha hizo zilikuwa nyingi kwa kipindi hicho na klabu hiyo isingeweza kuzitoa.
Hata hivyo, alisema Simba walimshangaza kwa kukubali masharti hayo, wakamkabidhi nusu ya fedha taslimu huku zilizo salio wakimwandikia hundi ili akalichukue benki.
“Simba walitaka kunisajili. Nikawatajia Sh45,000 nikijua hawawezi kunipa, lakini walinipa nusu taslimu na zilizobaki wakaniandikia hundi,” alisimulia Mkwasa.
Nguli huyo alisema wakati akiwa Uganda na kikosi cha timu ya taifa, alikutana na aliyekuwa Mwenyekiti wa vilabu vyote wakati huo, ambaye alimuuliza kama ni kweli alikuwa amesaini Simba.
Baada ya Mkwasa kukiri, mwenyekiti huyo alimuuliza ni timu ipi aliyokuwa anatamani kuichezea kati ya Simba na Yanga. Mkwasa bila kusita alijibu kuwa moyo wake ulikuwa Yanga.
Kutokana na jibu hilo, mwenyekiti huyo alipiga simu Radio Tanzania na kutangaza kuwa licha ya Mkwasa kusajiliwa na timu zote mbili, uamuzi wake ni kwamba aendelee kuichezea Yanga. Kauli hiyo ilimaliza mjadala wa usajili wake.
Baada ya uamuzi huo, Simba walimtaka Mkwasa arejeshe fedha walizokuwa wamempa. Kufikia wakati huo alikuwa tayari ametumia fedha taslimu alizopokea, lakini hakuwa amezichukua fedha za hundi benki.
Kutokana na hali hiyo, Simba walizuia hundi hizo zisilipwe na fedha zilizokuwa zimebaki zikarejeshwa kwenye akaunti ya klabu.
Akikumbuka tukio hilo, Mkwasa alisema baada ya kubaki Yanga, baadhi ya watu wa Simba walimuita “mwizi”, tukio ambalo limeendelea kubaki sehemu ya historia ya ushindani mkali kati ya watani hao wa jadi.

Related Articles

Back to top button