Nyumbani

Manara amtaka Samatta kurejea Afcon

DAR ES SALAAM: MSEMAJI wa timu za taifa, Haji Manara, amemuomba nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta, kuendelea kulitumikia taifa hadi AFCON 2027, akisema uzoefu wake wa soka la kimataifa unaweza kuwa silaha muhimu kwa kikosi hicho.

Hivi karibuni Samatta alitangaza kustaafu soka kwa kutocheza timu ya taifa hatua ambayo ilipingwa na wadau wengi wakimtaka asubiri mpaka Afcon mwakani imalizike.

Akizungumza na waandishi wa Habari leo Manara amesema uwepo wa Samatta ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo unaweza kuwapa hamasa wachezaji vijana hata kama hatakuwa na nguvu sawa na miaka yake ya awali.

“Samata, tunakuomba ahirisha hiyo wazo lako mpaka baada ya AFCON. Uwepo wako una faida kubwa. Unaweza kuwapa hamasa wenzako kwa sababu wewe ndiye nahodha,” amesema.

Amesema Samatta ni miongoni mwa wachezaji wachache watanzania waliowahi kufikia kiwango cha juu katika soka la kimataifa, akitaja mafanikio yake akiwa na TP Mazembe pamoja na uzoefu wa kucheza katika ligi mbalimbali za Ulaya.

Manara ameongeza kuwa uzoefu huo unamfanya Samatta kuwa zaidi ya mchezaji ndani ya kikosi, akisema anaweza pia kuwa kama kocha msaidizi kwa namna anavyoweza kuwashauri na kuwahamasisha vijana.

“Umetumikia taifa kwa muda mrefu na umeonesha thamani ya mpira, nidhamu na umeonesha mchezaji anatakiwa kuishi vipi. Vijana wanakuangalia wewe,” amesema.

 

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button