Tenisi U-12 yawasha moto Dar

DAR ES SALAAM: KOCHA wa timu ya taifa ya tenisi, Hassan Chande, amesema ushindani mkali unatarajiwa katika mashindano ya tisa ya kimataifa ya tenisi kwa vijana wenye umri chini ya miaka 12, yanayoshirikisha mataifa nane kutoka Afrika Mashariki na Kati.
Chande amesema kikosi chake kimejiandaa vyema kwa mashindano hayo na kina morali kubwa ya kupambana ili kuhakikisha Tanzania inafanya vizuri mbele ya mashabiki wa nyumbani.

Mashindano hayo yalianza jana, Julai 29, 2026, katika viwanja vya Gymkhana Club, Dar es Salaam, yakitarajiwa kuhitimishwa Agosti 2, mwaka huu.
Akizungumza kuhusu maandalizi ya timu yake, Chande amesema ushindani utakuwa mkubwa kutokana na ubora wa wachezaji kutoka mataifa mbalimbali, lakini Tanzania iko tayari kupambana kuwania ubingwa.
Mashindano hayo yamewakutanisha vijana kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Seychelles, Comoro, Burundi na Eritrea, huku yakilenga kukuza vipaji vya vijana na kuongeza ushindani wa mchezo wa tenisi katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Mbali na kuwania ubingwa, mashindano hayo yanatoa fursa kwa vijana kujifunza kupitia ushindani wa kimataifa na kujenga uzoefu muhimu katika hatua za mwanzo za safari zao za kimichezo.
Mwisho




