Nyota watatu Singida kumfuata Kibu

DAR ES SALAAM: NYOTA watatu wa Singida Black Stars, Emmanuel Keyekeh, Arthur Bada na Damaro Mohammed wamepwa uraia wa Tanzania baada ya wachezaji hao kuvutiwa na mandhari ya Tanzania.
Keyekeh raia wa Ghana, Bada kutoka Ivory Coast na Damaro (Guinea) wamepewa uraia wa Tanzania, tukio hilo lilitokea pia mwaka 2021 kwa mshambuliaji wa Simba, Kibu Denis kupewa uraia.
Ofisa Habari wa Singida Black Stars, Hussein Masanza amesema uongozi wa timu hiyo hauna mamlaka yoyote ya kumbadilisha uraia mchezaji au mfanyakazi yoyote wa kigeni.
“Wachezaji wetu watatu wamevutiwa na maisha ya Tanzania na wameomba uraia, wamefuata utaratibu zote uhamiaji kwa sababu suala la kubadili uraia na mambo binafsi, klabu tulishirikiana pale walipoomba msaada,” amesema.
Masanza amesema kutokana na maombi hayo klabu imeona ni faida kwa nchini waliwaunga mkono katika kila hatua ambayo walikuwa wakihitaji kutoka kwa uongozi wa timu hiyo.
“Nathibitisha hilo jambo limeshakamilika na kwetu haitagonga mwamba juu ya usajili wetu wa dirisha dogo, hawajavunja sheria tunaamini wachezaji wetu tumewapa ushirikiano wa kupata uraia wa Tanzania kama wachezaji wa timu nyingine walivyofanya,” amesema.
Miaka minne nyuma kulikuwa na ngumzo baaada ya kuibuka kwa utata wa uraia wa Kibu Denis aliyejiunga Simba akitokea Mbeya City ya Mbeya huku akidaiwa kuwa nyota huyo alikuwa raia wa Jamhuri wa Kidemokrasia ya Congo (DRC), lakini amekuwepo nchini Tanzania tangu mwaka 1998, akiwa na umri wa miaka sita, baada ya wazazi wake kukimbia machafuko ya kisiasa nchini humo.