Sowah atoa onyo: naja na kasi mpya katika mbio za kiatu cha dhahabu

DAR ES SALAAM: MSHAMBULIAJI mpya wa Singida Black Stars, Jonathan Sowah, ameweka wazi dhamira yake ya kutikisa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa ushindani mkali katika mbio za kuwania Kiatu cha Dhahabu msimu wa 2024/2025.
Sowah, ambaye alijiunga na Singida Black Stars wakati wa dirisha dogo la usajili, tayari ameonesha makali yake kwa kufunga mabao saba katika mechi sita alizocheza.
Akizungumza kuhusu malengo yake, mshambuliaji huyo amesema hana muda wa kupoteza na anataka kusaidia timu yake kupata matokeo bora huku akihakikisha anasalia kwenye orodha ya wafungaji bora.
“Nilipofika Tanzania, nilitazama msimamo wa wafungaji na nikamwona Elvis Rupia akiwa kinara. Sasa Jean Charles Ahoua wa Simba anaongoza mbio hizi, lakini mimi sijaja kuwa mshabiki, nimekuja kupambana,” amesema Sowah.
Kwa sasa, kiungo mshambuliaji wa Simba, Jean Charles Ahoua, ndiye anayeongoza chati ya wafungaji akiwa na mabao 12, akifuatiwa na Clement Mzize na Prince Dube wa Yanga, wenye mabao 10 kila mmoja.
Steven Mukwala (Simba) na Elvis Rupia wanashikilia nafasi ya tatu kwa mabao tisa, huku Leonel Ateba (Simba) na Peter Lwasa wakiwa na mabao nane. Sowah anashikilia nafasi ya tano kwa mabao saba, sawa na Stephane Aziz Ki wa Yanga.