Nyekundu na nyeupe zaipamba Moro
MOROGORO:MJI wa Morogoro umetawaliwa na rangi nyekundu na nyeupe baada ya Klabu ya Simba kuwasili katika mkoa huu kwa ajili ya uzinduzi rasmi wa wiki ya Simba na jezi zinazotumika kwa msimu ujao.
Msafara huo kutoka Dar es Salaam umeanza saa 12:00 alfajiri na kuwasili Stesheni ya Morogoro saa 1:30 kwa treni ya SGR, wakiwa mashabiki na Wananchama wa Simba wakiongozwa na Ofisa Mtendaji wa Klabu hiyo Imani Kajula na Mkuu wa Kitengo cha mawasiliano, Ahmed Ally.
Mbali na mashabiki kujitokeza kwa wingi lakini suala la usalama Barabarani umekuwa mzuri kwa kutokuwepo kwa foleni licha ya wingi wa magari ya mashibiki wa Simba.
Katika uzinduzi huo Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally amemtambulisha msanii wa Muziki wa kizazi kipya Ali Kiba atakuwa msanii ambaye ataburudisha siku ya kilele cha Simba Agosti 3,2024, Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam.
Katika kilele hicho Simba itakuwa na mechi ya kirafiki dhidi ya APR FC ya Rwanda, ukiwa ni mchezo wa kujipima nguvu kabla ya kucheza nusu fainali ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga, Agosti 8, mwaka huu, katika dimba la Benjamin Mkapa.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa zamani wa Simba , Hassan Dalali amemuomba Mtendaji Mkuu wa Simba,Imani Kajula kukutana na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kushirikiana katika ujezi wa Uwanja wa Jamhuri kuwa sehemu ya uwanja wao wa nyumbani.
“Nawapa salamu majirani zetu na wakumbuke kuwa Agosti 8, ya kila mwaka ni kilele cha Simba lakini tarehe hiyo ndio tunakutana nao, tumejiandaa vizuri na timu ipo kambini Misri kwa ajili ya msimu mpya,” amesema Dalali.