Muziki

Sony Music, Bongo Records kupeleka urithi wa Bongo Flava duniani

DAR ES SALAAM: KAMPUNI ya kusimamia na kusambaza kazi za muziki, Sony Music Entertainment, imetangaza ushirikiano na Bongo Records ya Tanzania, inayomilikiwa na mtayarishaji wa muziki Paul ‘P Funk’ Majani, kwa lengo la kupeleka historia ya Bongo Flava kwenye majukwaa ya kidijitali duniani.

Ushirikiano huo, uliotangazwa jijini Dar es Salaam, Agosti 6, 2026, unatarajiwa kufungua ukurasa mpya katika uhifadhi, usambazaji na uendelezaji wa urithi wa muziki wa Bongo Flava, kwa kuwezesha nyimbo, EP na albamu zilizotengenezwa chini ya Bongo Records kupatikana kwa urahisi kwa wasikilizaji wa kimataifa.

Katalogi hiyo inajumuisha kazi za baadhi ya wasanii waliotoa mchango mkubwa katika historia ya Bongo Flava, akiwemo Juma Nature, Professor Jay, marehemu Ngwair, Ferooz, Inspector Haroun, Fid Q na TMK Wanaume, pamoja na wasanii wengine.

Bongo Records, iliyoanzishwa na mtayarishaji Paul ‘P Funk’ Majani, ilikuwa miongoni mwa nguzo muhimu katika ukuaji wa Bongo Flava kuanzia miaka ya 1990, kipindi ambacho muziki huo ulianza kujenga utambulisho wake kupitia mchanganyiko wa Hip Hop, R&B, Rhumba, Pop, Taarab na mashairi ya Kiswahili.

Akizungumza kuhusu ushirikiano huo, P Funk amesema makubaliano hayo ni hatua ya kihistoria katika kuhakikisha kazi za muziki zilizobeba utamaduni, maisha na simulizi za Tanzania zinawafikia wasikilizaji wapya duniani.

“Nyimbo hizi ni zaidi ya muziki—ni ramani ya mapigo ya Tanzania,” amesema P Funk, akieleza kuwa kuziweka kazi hizo kwenye majukwaa ya kimataifa kutasaidia kuzihifadhi na kuhakikisha urithi wa Bongo Flava unaendelea kufahamika na kizazi kipya.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Sony Music Africa, Sean Watson, amesema Bongo Flava ni miongoni mwa harakati muhimu za kitamaduni barani Afrika, hivyo ushirikiano huo utasaidia kuheshimu msingi uliowekwa na waanzilishi wa muziki huo huku ukiandaa mazingira ya ukuaji wake zaidi kimataifa.

Amesema hatua hiyo pia inalenga kuhakikisha muziki wa kizazi kilichotangulia unapata nafasi ya kufikiwa na hadhira mpya katika zama ambazo majukwaa ya kidijitali yamekuwa sehemu muhimu ya usambazaji wa muziki duniani.

Ushirikiano huo unaonekana kuwa hatua muhimu katika safari ya Bongo Flava kuelekea hadhira ya kimataifa, huku ukitoa fursa kwa kizazi kipya kugundua upya kazi zilizochangia kuandika historia ya muziki huo nchini Tanzania.

Related Articles

Back to top button