Ligi Kuu

Ahmed Ally awataka mashabiki Simba kuacha taharuki 

DAR ES SALAAM: BAADA ya mshambuliaji Selemani Mwalimu kutambulishwa rasmi na Yanga asubuhi ya leo, Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amewataka mashabiki wa klabu hiyo kuacha taharuki na kuelekeza nguvu zao kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii unaotarajiwa kuchezwa kesho.
Mwalimu, ambaye alikuwa mshambuliaji wa Simba, ametambulishwa na Yanga na hivyo kuibua mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki wa Simba kuhusu namna alivyohamia kwa watani wao wa jadi.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao, Ahmed Ally amekiri kuwa kutambulishwa kwa Mwalimu Yanga kumeleta taharuki kwa baadhi ya Wana Simba, lakini amesisitiza kuwa kwa sasa hataki kuingia katika maelezo ya kilichotokea.
“Wengi tumeingia kwenye taharuki baada ya kuona aliyekuwa mshambuliaji wetu akitambulishwa klabu nyingine. Kwanza niwape pole Wana Simba kwa taharuki hii. Sipo hapa kujielezea nini kimetokea,” aliandika Ahmed.
Badala yake, kiongozi huyo amewataka mashabiki wa Simba kuelekeza akili na nguvu zao kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga akisisitiza kuwa klabu hiyo inalenga kuanza msimu mpya kwa kutwaa taji hilo baada ya kulikosa kwa misimu miwili.
“Kitu muhimu zaidi kwa sasa tuwekeze nguvu kwenye mchezo wetu wa kesho wa Ngao ya Jamii. Hakuna tunachokihitaji zaidi ya ushindi,” amesema.
Ahmed ameongeza kuwa huu ni wakati sahihi kwa Simba kurejesha taji hilo na kuanza msimu kwa ushindi.
Kauli hiyo imekuja wakati mjadala kuhusu kuondoka kwa Mwalimu kwenda Yanga ukiwa bado moto, huku mashabiki wa Simba wakisubiri ufafanuzi zaidi kuhusu sababu za mshambuliaji huyo kuachana na klabu hiyo na kujiunga na wapinzani wao wakubwa.

Related Articles

Back to top button