Nyumbani

TFF yazindua tiketi kidijitali Simba, Yanga

DAR ES SALAAM: SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limezindua mfumo mpya wa kidijitali wa ununuzi wa tiketi kuelekea mchezo wa Ngao ya Jamii 2026, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wake kwa mashabiki.
Kupitia mfumo huo, mashabiki watatakiwa kuingia kwenye kwenye tovuti maalumu na kuchagua mchezo wa Ngao ya Jamii 2026, kisha kuchagua eneo wanalotaka kukaa na kukamilisha malipo kwa njia za kidijitali.

Akizungumza wakati wa kutangaza mfumo huo, Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF Clifford Ndimbo amesema mfumo huo mpya umeanzishwa ili kurahisisha mchakato wa ununuzi wa tiketi na kuingia uwanjani.

Amesema mashabiki watakapokamilisha ununuzi, tiketi zao zitakuwa na majina yao na zitatumwa kwa njia ya kidijitali, hivyo hawatalazimika kuchapisha tiketi hizo.

“Kwa sasa tiketi zitakuwa zinapatikana kidijitali. Ukimaliza mchakato wote, utapata tiketi yako ambayo itakuja kuscaniwa wakati unaingia uwanjani,” amesema.

Mfumo huo pia umewekewa kikomo cha ununuzi wa tiketi nne kwa kutumia namba moja ya simu ya mkononi, huku malipo yakiruhusiwa kupitia mitandao mbalimbali ya simu.

Kwa mujibu wa TFF, bei za tiketi kwa mchezo huo zimewekwa katika madaraja tofauti, ikiwamo Sh10,000, Sh20,000, Sh30,000 kwa baadhi ya maeneo, huku VIP A ikiwa Sh50,000.

Hatua hiyo ni sehemu ya maboresho ya teknolojia katika uuzaji na udhibiti wa tiketi, huku TFF ikitarajia mfumo huo kusaidia kupunguza usumbufu kwa mashabiki na kurahisisha udhibiti wa uingiaji uwanjani.

Mchezo wa Ngao ya Jamii 2026 wa Simba dhidi ya Yanga utachezwa kesho kutwa Zanzibar.

 

Related Articles

Back to top button