Mngqithi: Makosa ya kizembe yalituua, naomba radhi

DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa Yanga, Manqoba Mngqithi, amekiri makosa ya kizembe ndiyo yaliyoigharimu timu yake katika kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Aigles du Congo, akiomba radhi na kuwataka mashabiki kutokuwa na hofu akiahidi kuwa timu hiyo itakuwa imara zaidi msimu mpya.
Yanga ilifungwa mabao 2-1 jana kwenye Uwanja wa Uhuru, huku Mngqithi akikiri timu yake ilianza vizuri na kutengeneza nafasi, lakini kushindwa kuzitumia pamoja na makosa ya kiulinzi kuliwapa wapinzani nafasi ya kupata ushindi.
“Tulianza mchezo vizuri. Tulionekana kuwa hatari kupitia presha ya juu na ‘counter-pressing’, lakini hatukutumia nafasi zetu. Tulifunga bao zuri kupitia penalti, ambalo lilitokana tena mashambulizi ya haraka,” amesema Mngqithi.
Amesema Yanga ilifanya kosa kubwa lililozaa bao la kwanza la Aigles du Congo baada ya mpira kurudishwa kwa kipa bila kuwa na ulinzi wa kutosha kutoka safu ya kati.
“Kwa kweli lilikuwa bao la kizembe sana. Mpira ulirudishwa kwa kipa, lakini hakukuwa na msaada kutoka kwa safu ya kati. Yao aliyekuwa amerudisha mpira alikuwa chini ya presha na akapiga mpira mrefu. Okello alipokuwa akijaribu kuupokea, mwenzake akamsumbua na hilo likawapa wapinzani nafasi ya kushambulia,” amesema.
Mngqithi amesema kipindi cha pili Yanga ilianza vizuri na ilionekana inaweza kupata bao wakati wowote kutokana na nafasi ilizotengeneza katika eneo la mwisho, lakini uzembe katika umaliziaji uliendelea kuwa tatizo.
Amesema bao la pili lilitokana pia na kosa la mchezaji kijana aliyekuwa nje ya nafasi yake, jambo lililowapa Aigles du Congo nafasi ya kuadhibu.
Licha ya kipigo hicho, Mngqithi amesema amefurahishwa na mambo mazuri aliyoyaona kutoka kwa timu yake, akisisitiza kuwa mashabiki wataiona Yanga tofauti katika mchezo wao ujao.
Amesema katika mchezo huo alilazimika kugawa vikosi ili kuwapa nafasi wachezaji mbalimbali, hasa vijana, lakini mchezo ujao utakuwa wa ushindani zaidi kwa kikosi cha kwanza.
“Unaweza kutarajia mchezo mzuri sana Jumatano. Tulilazimika kusawazisha vikosi viwili. Nimefurahishwa na vijana waliocheza, lakini Jumatano itakuwa biashara halisi kwa kikosi cha kwanza kuonesha uwezo wake,” amesema.
Kocha huyo amesema Yanga ina kikosi imara na kwamba mashabiki wanapaswa kuwa na subira kwa kuwa malengo yao ni kufanya vizuri katika mashindano yote, ikiwamo Ligi ya Mabingwa Afrika.
Akizungumzia Tamasha la Yanga, Mngqithi aliwashukuru mashabiki kwa kujitokeza kwa wingi na kuendelea kuishangilia timu licha ya matokeo.
“Walitupa mazingira mazuri. Pia naomba radhi kwa kutowapa matokeo baada ya kujitokeza kwa wingi namna hiyo. Walikuwa pamoja nasi wakati wa kipindi kigumu na kizuri,” amesema.




