Dilunga, Kichuya waipa ushindi wa kwanza JKT Tanzania
DAR ES SALAAM: Hatimaye Maafande wa JKT Tanzania wamefanikiwa kupata ushindi wao wa kwanza katika Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara baada ya kuwatandika wagosi wa kaya Coastal Union mabao mawili kwa moja.
JKT wamepata ushindi huo nyumbani katika dimba la Meja Jenerali Isamuhyo uliopo mbweni nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam katika mchezo uliopigwa leo Septemba 25 majira ya saa 8 mchana.
Magoli ya JKT Tanzania yamefungwa na mchezaji wa zamani wa wekundu wa Msimbazi Simba Hassan Dilunga kwa mkwaju wa penalti mnamo dakika ya 14 kabla ya John Makwata wa Coastal Union kusawazisha dakika ya 27 na baadaye Shiza Kichuya kuingia kambani mnamo dakika 48 kipindi cha pili.
Huu unakuwa mchezo wa kwanza kwa maafande hao kupata ushindi huku wakipata sare kwenye michezo minne iliyopita.
Hali ni mbaya zaidi kwa Coastal Union ambao katika michezo mitano ya Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara baada ya kutandikwa mechi nne na kutoa sare moja pekee.