World Cup

Baba ake Neymar amkingia kifua mwanae

..mwanangu ubora haumuliwi kwa umri wala mazingira

Baba wa nyota wa Brazil, Neymar Jr., Neymar Santos Sr. amemtaka mwanawe asiache kucheza soka licha ya Brazil kutolewa na Norway katika hatua ya 16 bora ya Kombe la Dunia 2026.

Neymar Jr aliingia kipindi cha pili akitokea benchi na kufunga bao la kufutia machozi kwa mkwaju wa penalti, lakini halikutosha kuizuia Brazil kupoteza kwa mabao 2-1 na kuaga mashindano hayo.

Baada ya kipenga cha mwisho, Neymar Jr alionekana akilia na kusema safari yake katika timu ya taifa imefika mwisho.

“Kila kitu kimeishia hapa. Kilianza hapa MetLife Stadium, na nimemalizia hapa,” alisema Neymar Jr.

Nyota huyo wa Santos alicheza mechi yake ya kwanza kwa Brazil Agosti 2010 dhidi ya Marekani katika uwanja huo huo wa MetLife Stadium.

Takribani miaka 16 baadaye, ameonekana kuhitimisha safari yake ya kimataifa akiwa katika uwanja huo huo.

Neymar mwenye umri wa miaka 34 anaondoka akiwa mfungaji bora wa muda wote wa Brazil akiwa na mabao 80.

Katika kipindi chake na timu ya taifa, alitwaa taji la Copa América pamoja na medali ya dhahabu ya Michezo ya Olimpiki, lakini hakuwahi kutimiza ndoto yake ya kutwaa Kombe la Dunia.

Tangu Brazil ilipoondolewa kwenye mashindano hayo, Neymar amebaki kimya kwenye mitandao ya kijamii, hali iliyoibua hisia kuwa huenda amefunga rasmi ukurasa wa kuitumikia timu ya taifa.

Hata hivyo, baba yake, Neymar Sr., amempa ujumbe wa kumtia moyo na kumtaka aendelee na maisha yake ya soka.

“Oh, mwanangu… Ni safari ya kipekee. Njia nzuri, yenye changamoto nyingi na maumivu mara kadhaa, lakini pia imejaa baraka zisizo na kikomo. Uamuzi uliofanywa leo hauwezi kufafanua historia yako yote. Ndoto ambayo haijatimia bado haimaanishi kwamba imekufa,” aliandika Neymar Sr.

Aliendelea kwa kumhimiza mwanawe arejee kufurahia mchezo alioupenda na asiangalie umri wala changamoto alizopitia.

“Ninapoangalia mbele bado nina imani ileile. Ubora hauamuliwi na umri wala mazingira. Kama baba yako, ninakuomba jambo moja tu… Mwanangu, endelea kucheza soka. Rudisha furaha yako ndani ya mchezo,” alisisitiza.

Miaka ya karibuni, Neymar amekumbwa na changamoto za majeraha na kuporomoka kwa kiwango, hasa baada ya kupata jeraha kubwa la goti mwaka 2023. Kabla ya kuitwa kwa mshangao kwenye kikosi cha Kocha Carlo Ancelotti kwa Kombe la Dunia 2026, alikuwa hajaitumikia Brazil kwa takribani miaka mitatu.

Related Articles

Back to top button