Okello: Tulipaswa kufunga mabao zaidi

DAR ES SALAAM: KIUNGO mshambuliaji wa Yanga Allan Okello amesema ushindi wa bao 1-0 walioupata dhidi ya KMC jana haukuwa mwepesi kutokana na timu hiyo kukosa nafasi nyingi za wazi kipindi cha kwanza cha mchezo.
Okello ambaye ndiye aliyefunga bao pekee la ushindi amesema walitengeneza nafasi nyingi lakini walishindwa kuzitumia kabla ya kurejea kipindi cha pili kwa nguvu zaidi na kupata bao muhimu lililowapa pointi tatu.
Amesema kipindi cha kwanza walipaswa kuwa wamefunga mabao matatu kutokana na nafasi walizozalisha, jambo lililowafanya wachezaji kuwa na huzuni ndani ya vyumba vya kubadilishia nguo wakati wa mapumziko.
Amesema kipindi cha pili KMC waliongeza umakini na kuziba nafasi nyingi tofauti na ilivyokuwa mwanzoni mwa mchezo, hali iliyowalazimu kujaribu mashuti ya mbali pamoja na kusubiri nafasi chache ndani ya boksi.
Okello amesema jambo muhimu kwao si tuzo binafsi wala nani anakuwa mchezaji bora wa mechi, bali ni kuhakikisha timu inapata pointi tatu katika kila mchezo.
Amesema wanaendelea kuchukua mechi moja baada ya nyingine katika mbio za ubingwa huku akiwashukuru mashabiki kwa kuendelea kujitokeza kuwapa sapoti ambayo huwapa morali na kujiamini zaidi uwanjani.
“Tunawahitaji mashabiki nyuma yetu kwa sababu wanatupa nguvu ya kupambana na kupata pointi tatu kila siku,” amesema Okello.



