Karia: VAR ligi kuu bado kwanza
DAR ES SALAAM: Rais wa shirikisho la soka nchini TFF Wallace Karia amesema ni ngumu kutumia teknolojia ya usaidizi wa muamuzi kwa njia ya video VAR msimu huu kutokana na sababu za kiusawa kwa vilabu vyote vya ligi kuu ya NBC Tanzania Bara.
Karia ameyasema hayo wakati akijibu swali la mwandishi wa habari juu ya matumizi ya teknolojia hiyo kwenye michezo ya Ligi kuu wakati wa ufunguzi wa kozi ya VAR kanda ya CECAFA iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
“Tusidanganyane huwezi kuwa na seti kwa asilimia 60 ya mechi, lakini ili uweze kuja kufanya jambo kuna kitu kinaitwa equity ni lazima kuwe na uwiano sawa. Kwa hiyo hiyo asilimia 40 wengine watapata maamuzi ambayo sio ya upande wao”.
“Kwa hiyo leo sisi tunafanya mafunzo ili kukiwa na mashindano labda ngao ya jamii ya mechi tatu, nne tunaweza kufanya iyo lakini kwenye ligi bado mpaka tuwe na uhakika wa kutosheleza mechi zote” amesema Karia
Ikumbukwe mwanzoni mwa msimu huu kulikuwa na kauli za huenda teknolojia hiyo inayoondoa utata wa maamuzi ingetumika kwenye asilimia 60 ya mechi za ligi kuu msimu huu kikwazo pekee kikitajwa kuwa vibali kutoka shirikisho la mpira wa miguu duniani FIFA.