Ni Azam FC, TRA kusaka pointi tatu Leo

ARUSHA: MACHO na masikio ya wadau wa soka leo yataelekezwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha ambapo TRA United itaikaribisha Azam FC katika mchezo muhimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara wenye vita ya pointi tatu na nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi.
Azam FC wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa nafasi ya tatu na pointi 43, huku wakibebwa na mwendelezo mzuri wa matokeo baada ya kushinda michezo mitatu na kutoka sare mbili katika mechi zao tano zilizopita.
Kwa upande wa TRA United, waliopo nafasi ya sita na pointi 30, ushindi wa leo unaweza kuwapa matumaini mapya ya kuwania nafasi nne za juu.
Ofisa Habari wa TRA United, Christina Mwagala amesema kikosi chao kiko tayari kupambana kuhakikisha kinaondoka na ushindi mbele ya Azam FC.
“Wanaume wa Dar Azam FC wanaziacha pointi tatu. Malengo yetu ni kuhakikisha tunapata ushindi na kuingia katika nne bora za juu na inawezekana kwani michezo yote iko chini yetu,” amesema Mwagala.
Kwa upande wa Azam FC, Ofisa Habari wa klabu hiyo Hasheem Ibwe amesema wanatarajia ushindani mkubwa lakini dhamira yao ni kuendelea kulinda rekodi yao nzuri.
“Tunategemea ushindani mkubwa, hatujapoteza mchezo wowote katika mwendelezo wetu wa hivi karibuni na tunazitaka pointi tatu,” amesema Ibwe.




