Kasongo ataka nafasi zaidi kwa vijana NBCPL

DAR ES SALAAM: OFISA Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu (TPLB), Almas Kasongo ametaja moja ya kanuni iliyoongezwa kwa msimu mpya ni kila timu lazima ipandishe wachezaji wawili kutoka timu za vijana.
Msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara unatarajiwa kuanza kutimua vumbi Agosti 16 mwaka huu, na Alhamisi ya keshokutwa kutakuwepo na mchezo wa nusu fainali ya Ngao ya Hisani utakaochezwa Visiwani Zanzibar na Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam.
Kasongo amesema kuna kanuni ambazo zimeboreshwa na zingine kuondolewa na nyingine ni mpya ikiwemo suala la kuwasaidia wachezaji kutoka timu za vijana kupata nafasi kuwepo katika benchi la ufundi la timu kubwa za ligi kuu.
“Tumeweka kanuni kwa ajili ya kuwapa ushindani na uzoefu wakiwa wadogo na kumfanya kukuwa katika ushindani mkubwa na kupata uzoefu kuja kusaidia hapo baadae,” amesema Kasongo.
Amesisitiza kuwa msimu wa 2024/25 watakuwa wakali na bodi ya ligi ni chombo cha klabu za Tanzania na wamewaeleza kuhusu kanuni hizo ikiwemo kutofumbia macho suala la miundo mbinu.
“Hatutaruhusu kutumika kwa uwanja usiokuwa na miundo mbili yote ikiwemo ubora wa benchi la ufundi, kuwepo kwa vyumba vya kubadilishia nguo kwa wachezaji na kuwepo kwa viti 3000 katika majukwaa wanaokaa mashabiki,” amesema Kasongo.