Navas atimkia Amerika Kusini

ROSARIO:Keylor Navas, kipa mkongwe wa Costa Rica, amejiunga rasmi na klabu ya Newell’s Old Boys ya Argentina kwa uhamisho huru. Navas, mwenye umri wa miaka 38, alitangaza kujiunga na klabu hiyo kwa mkataba wa hadi Juni 2026 baada ya kuondoka Monza alikocheza kwa muda mfupi.
Kipa huyo aliyejizolea sifa kwa wepesi na uwezo wa kuokoa mashuti makali alijizolea umaarufu akiwa Real Madrid, akisaidia klabu hiyo kushinda mataji kadhaa ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Baada ya mafanikio hayo, alihamia Paris Saint-Germain (PSG) ambako alidumisha nafasi yake kama mmoja wa makipa bora duniani.
Navas anatarajiwa kuwa nguzo muhimu kwa Newell’s Old Boys kutokana na uzoefu na uongozi wake, huku akijulikana kwa reflexi za haraka na udhibiti wa eneo la penalti. Ujio wake ni hatua kubwa kwa klabu hiyo inayotafuta kuimarisha kikosi chao.