Haaland nje hadi mwisho wa Januari
MSHAMBULIAJI wa Manchester City, Erling Haaland huenda akakaa nje ya uwanja hadi mwisho wa mwezi huu kutokana na majeraha.
Jeraha la mguu limemweka Haaland mwenye umri wa miaka 23 nje ya uwanja tangu City ilipofungwa bao 1-0 na Aston Villa Desemba 6, 2023 katika mchezo wa Ligi Kuu England.
Ilitumainiwa mshambuliaji huyo kinara wa City angerejea uwanja wakati wa michuano ya Kombe la Dunia la Klabu Desemba, 2023 lakini jeraha hilo halijapona.
“Ameumia mfupi. Kupona kunahitaji muda mrefu. Tunatumaini mwisho wa mwezi atakuwa tayari. Mwanzoni haikutarajiwa kuwa hivi,” amesema Kocha wa City, Pep Guardiola.
Haaland, mchezaji wa Kimataifa wa Norway amefunga mabao 19 katika mechi 22 msimu huu.
Iwapo hatacheza muda uliobaki mwezi huu, atakosa mechi ya Kombe la FA ugenini Januari 26 dhidi ya Tottenham na mchezo wa Ligi Kuu nyumbani Januari 31 dhidi ya Burnley.
City haijapoteza katika michezo nane ambayo Haaland amekosa ikiwemo ya ubingwa wa Kombe la Dunia la Klabu na ipo nyuma ya Liverpool kwa pointi tano EPL huku ikiwa nyuma mchezo mmoja ambao leo inacheza na Newcastle United.