Nancy Sumari aipeperusha bendera ya Tanzania kimataifa

DAR ES SALAAM: Miss Tanzania 2006 na Miss World Africa, ambaye kwa sasa ni mbunifu wa teknolojia, Nancy Sumari, ameendelea kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania kimataifa baada ya kushinda tuzo ya Ubunifu kutoka Zero Project nchini Austria.
Nancy ametunukiwa tuzo hiyo kwa kutambua mchango wake kupitia Taasisi ya JengaHub katika kuendeleza elimu jumuishi kwa watoto wenye ulemavu nchini Tanzania.
Akiwa Mkurugenzi wa JengaHub, Nancy amepokea nishani ya heshima pamoja na taasisi nyingine zikiwemo Child Support Tanzania na Kyaro Assistive Tech, zilizotambuliwa kwa ubunifu wao katika kusaidia jamii ya watu wenye ulemavu.
Kupitia taarifa yake, Nancy amesema JengaHub imebuni Kalimani App, jukwaa la kujifunza kidijitali linalotumia teknolojia ya akili mnemba (AI) kusaidia watoto wenye ulemavu wa kusikia kujifunza kusoma, kuandika, kuhesabu pamoja na ujuzi wa kidijitali.
“Kalimani App hufundisha kwa kutumia lugha ya alama ya Tanzania na inatarajiwa kutumika katika shule za kawaida na maalum katika mikoa sita nchini,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Vyeti vya pongezi vilitolewa Februari, 2026, wakati wa Mkutano Mkuu wa Zero Project uliofanyika jijini Vienna, Austria.
Kupitia ushindi huo, Nancy ameendelea kuwa chachu ya mabadiliko katika sekta ya elimu na teknolojia, akionesha kuwa ubunifu wa Kitanzania unaweza kutambulika na kuheshimiwa katika jukwaa la kimataifa.




