Nadal akubali yaishe, aachia ujumbe mzito

BINGWA mara 22 wa Grandslam Rafael Nadal ametangaza kustaafu kucheza tenisi baada ya michuano ya Davis Cup ya mwezi ujao. Mtaalamu huyo wa rackets amefanya maamuzi hayo baada ya kuandamwa na majeruha siku za hivi karibuni.
Mhispania huyo mwenye miaka 38 alitangaza uamuzi huo katika video aliyoichapisha katika mtandao wake wa X (zamani twitter). Uamuzi ambao umepokelewa kwa hisia tofauti na wapenzi wa mchzo huo duniani.
“Ni wazi kuwa ni uamuzi mgumu, ambao umenichukua muda mrefu kuufanya. Lakini, katika maisha haya, kila kitu kina mwanzo na mwisho. Na nadhani ni wakati mwafaka wa kumaliza kazi ambayo imekuwa ya muda mrefu na yenye mafanikio zaidi kuliko nilivyowahi kufikiria.” Amesema
“Najiona mwenye bahati sana kwa mambo yote ambayo nimepitia, nataka kuwashukuru wanamichezo na tasnia nzima ya tenisi, watu wote wanaohusika na mchezo huu, wenzangu wa muda mrefu, haswa wapinzani wangu wakubwa. Nimetumia muda mwingi nao na nimeishi nyakati nyingi ambazo nitakumbuka maisha yangu yote.”
Nadal ni mshindi wa mataji 22 ya Grandslam yakiwemo 14 ya French Open, 4 ya US Open, 2 ya Wimbledon na 2 ya Australian Open