Burudani

Mwana FA alitaka COSOTA kuchukua hatua maharamia wa vitabu

DAR ES SALAAM: NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’, ameitaka Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) kushirikiana na Chama cha Wachapishaji Tanzania (PATA) kuwasilisha taarifa za operesheni zilizofanyika na kesi zilizofunguliwa dhidi ya watu wanaojihusisha na uharamia wa kazi za maandishi.

Mwinjuma ametoa agizo hilo wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya 33 ya Kimataifa ya Vitabu Tanzania yaliyofanyika katika Viwanja vya Maktaba jijini Dar es Salaam, akisisitiza umuhimu wa kulinda kazi za waandishi na kuhakikisha sheria za hakimiliki zinatekelezwa.

Amesema pamoja na kuwa suala hilo halikuwekwa kwenye ajenda ya kikao kilichopangwa kufanyika kati yake na COSOTA, ameomba liingizwe ili kujadili hatua zilizochukuliwa dhidi ya wanaokiuka haki za waandishi na wachapishaji.

“Tuna kikao na COSOTA. Najua katika ajenda zetu hili suala hatukuliweka, ila naomba liweke kwenye ajenda zetu katika kikao tutakachokaa hivi karibuni,” amesema Mwinjuma.

Amesema vitabu si nyenzo za kujifunzia darasani pekee, bali pia ni hazina ya kumbukumbu za taifa, daraja linalounganisha vizazi na njia muhimu ya kukuza fikra, ubunifu na uwezo wa jamii kujielewa.

Ameeleza kuwa historia ya taifa haiwezi kuhifadhiwa na kurithishwa kwa ukamilifu bila maandishi, machapisho na taasisi zinazoyatunza. Kwa msingi huo, amesema kuendeleza utamaduni wa kusoma, kuandika, kuchapisha na kutunza vitabu ni sehemu muhimu ya kukuza elimu, Kiswahili, sanaa na utambulisho wa Mtanzania.

Mwinjuma pia amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, taasisi za elimu na utafiti, waandishi, wachapishaji na wasomaji katika kukuza Kiswahili, akibainisha kuwa lugha hiyo ina nafasi muhimu katika mawasiliano, elimu, utamaduni na utambulisho wa taifa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa PATA, Hermes Damian, ameiomba Serikali kuwekeza katika ujenzi wa Maktaba ya Kimataifa ya Kiswahili itakayohifadhi kazi zote za Kiswahili zilizokwishaandikwa na zinazoendelea kuandikwa ili zilindwe na kurithishwa kwa vizazi vijavyo.

Damian amesema maktaba hiyo itakuwa muhimu katika kuhifadhi urithi wa lugha ya Kiswahili na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama moja ya nchi zinazoongoza katika kuitunza na kuikuza lugha hiyo duniani.

Aidha, amependekeza kuanzishwa kwa jukwaa maalumu la Swahili Hall of Fame, litakalotambua mchango wa waandishi wakongwe na wanaochipukia katika kukuza Kiswahili na fasihi yake.

Amesema Serikali inapaswa kuweka utaratibu wa kuwatambua waandishi wa zamani na wa sasa waliochangia maendeleo ya lugha na fasihi ya Kiswahili, akieleza kuwa utambuzi huo utasaidia kuthamini mchango wao kwa taifa na kuhamasisha kizazi kipya cha waandishi.

Vilevile, Damian ameiomba Wizara kujenga maktaba ya kumbukumbu katika nyumba ya Shaaban Robert iliyopo Tanga ili kuhifadhi kazi zake na vitu vingine vya kihistoria alivyoviacha, hatua ambayo amesema inaweza kuongeza vivutio vya kiutamaduni na kifasihi katika jiji hilo.

Ameitaka pia Serikali kufufua Tuzo ya Shaaban Robert ya Fasihi iliyokuwa ikiratibiwa na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), pamoja na Tuzo ya Zeze ya Mfuko wa Utamaduni, na kutenga fedha za kuziendesha ili ziendelee kusaidia kuibua vipaji na kukuza lugha ya Kiswahili.

Katika hatua nyingine, mwenyekiti huyo amesisitiza umuhimu wa kuwa na sera ya vitabu na usomaji nchini, akisema sera hiyo itasaidia kujenga utamaduni wa Watanzania kusoma kwa ajili ya kupata maarifa, ujuzi na kufahamu urithi wa jamii zao, badala ya kusoma kwa madhumuni ya kupata elimu rasmi pekee.

Amesema kuwepo kwa sera hiyo kutatoa mwelekeo wa kuendeleza sekta ya vitabu na kuhamasisha usomaji katika jamii, huku akihimiza Serikali na wadau kuweka mazingira yatakayowezesha vitabu vya Kiswahili kuhifadhiwa, kuchapishwa na kupatikana kwa urahisi.

Related Articles

Back to top button