Afrika Mashariki

Adam: Serengeti boys tujipange upya

KIGALI: KOCHA wa timu ya taifa ya wavulana chini ya miaka 17 (Serengeti Boys), Adam Mbwana, amesema benchi la ufundi litarejea katika uwanja wa mazoezi kufanya marekebisho baada ya timu hiyo kutoka sare dhidi ya Somalia katika mchezo wa pili wa kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 kwa vijana, Kanda ya CECAFA.

Mchezo huo ulichezwa jana kwenye Uwanja wa Pele, Kigali nchini Rwanda.

Mbwana amesema mchezo huo umekuwa funzo kwa timu yake, hasa katika namna ya kumiliki mpira, kutengeneza nafasi na kukabiliana na timu zinazoshambulia kwa kasi.

Amesema Serengeti Boys haikuonesha kiwango kizuri ilipokuwa na mpira, ikishindwa kutumia nafasi na kukabiliana ipasavyo na presha ya Somalia, iliyocheza kwa nguvu na kuwapa wakati mgumu.

Ameeleza kuwa licha ya changamoto hizo, timu yake imeimarika katika ulinzi ikilinganishwa na mchezo uliopita, akiwapongeza wachezaji kwa namna walivyokabiliana na mashambulizi ya wapinzani, hasa kupitia mawinga wa kulia na kushoto.

“Ni lazima tukubali kwamba hatukuwa na mchezo mzuri sana, hasa tulipokuwa na mpira. Tulishindwa kufungua nafasi na kuzitumia vizuri. Somalia walikuwa wakali na tulishindwa kukabiliana nao ipasavyo,” amesema Mbwana.

Ameongeza kuwa benchi la ufundi litachambua mchezo huo na kufanya kazi katika maeneo yaliyoonekana kuwa na mapungufu, akiamini kuwa Serengeti Boys inaweza kuonesha kiwango tofauti katika mchezo unaofuata.

Kuhusu nafasi ya kufuzu hatua ya nusu fainali, Mbwana amesema timu hiyo italazimika kusubiri matokeo ya mchezo kati ya Kenya na Somalia ili kufahamu hatma yake katika kundi hilo.

Amesema endapo Serengeti Boys itafuzu, itatumia muda wa mapumziko kufanya mazoezi na kuboresha maeneo mbalimbali ya mchezo ili kuingia hatua ya nusu fainali ikiwa na maandalizi bora zaidi.

Related Articles

Back to top button