Singida Black Stars kuifuata Tusker Nairobi

ARUSHA: SINGIDA Black Stars imeelekeza nguvu katika mchezo wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Tusker FC ya Kenya, ikilenga kupata matokeo mazuri ugenini yatakayoipa nafasi ya kufuzu hatua ya makundi ya mashindano hayo.
Msemaji wa klabu hiyo, Hussein Massanza, amesema timu hiyo inalichukulia kwa uzito pambano hilo la raundi ya awali, akieleza kuwa michezo miwili dhidi ya Tusker ndiyo itakayoamua hatima yao katika mashindano ya CAF msimu huu.
Massanza amesema kikosi hicho kinatarajiwa kusafiri kutoka jijini Arusha kwenda Nairobi, Kenya, Oktoba 16, kwa ajili ya mchezo wa kwanza utakaochezwa Oktoba 18 katika Uwanja wa Nyayo.
Ameongeza kuwa maandalizi ya safari yanaendelea kuratibiwa na viongozi wa klabu, huku baadhi yao wakitangulia Nairobi kuhakikisha mahitaji muhimu ya timu yanakamilishwa kabla ya kuwasili kwa kikosi.
Massanza amesema benchi la ufundi linaendelea kuimarisha kikosi ili kiwe tayari kukabiliana na Tusker, akisisitiza kuwa lengo ni kupata matokeo mazuri katika mchezo wa kwanza kabla ya kurejea nyumbani kwa ajili ya mchezo wa marudiano.
Amesema Singida Black Stars inalenga kutumia uzoefu wake katika mashindano ya kimataifa ili kufikia hatua ya makundi kwa mara nyingine, huku ikitambua umuhimu wa michezo hiyo miwili katika kutimiza azma hiyo.




