Mastaa

Maria sasa ataka Chris Brown akamatwe

CALIFORNIA: ALIYEKUWA mfanyakazi wa nyumbani wa Chris Brown, Maria Avila, anataka mwimbaji huyo akamatwe kwa kutia ugumu kulipwa fidia ya Dola milioni 9 aliyoshinda mahakamani kufuatia kung’atwa na mbwa.

Kwa mujibu wa nyaraka zilizonaswa na Mtandao wa TMZ, Maria, ameiomba mahakama kutoa hati ya kukamatwa kwa Chris.

Amedai kuwa msanii huyo anakwepa kutoa tarehe ambazo angefika mahakamani na rekodi zake za benki, jambo ambalo lingemsaidia Maria kubaini namna ya kupata malipo yake.

Alisema taarifa ambazo Chris alitoa hazikuwa kamili na zinaibua mashaka kuhusu usahihi na ukamilifu wa taarifa alizotoa kuhusiana na vyanzo vya malipo vinavyotokana na ziara yake ya kimuziki inayoendelea.

Julai Mosi, mwaka huu, Maria alishinda kesi ya kulipwa fidia ya Dola milioni 9 baada ya kesi kusikilizwa na baraza la wazee wa mahakama.

Awali baada ya ushindi huo, Maria alipendekeza alipwe fidia hiyo kupitia mapato ya kwenye ziara ya msanii huyo, kitu ambacho kilipingwa vikali na Chris.

Maria alishambuliwa na mbwa mwaka 2020 wakati akitoa takataka nje katika jumba la kifahari la Chris lililopo jijini Los Angeles.

Related Articles

Back to top button