Muziki

Koffi Olomidé azua gumzo

....baada ya tukio lisilo la kawaida jukwaani

NAIROBI: MWANAMUZIKI mkongwe wa rhumba kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Koffi Olomidé, amezua mjadala mkali mitandaoni baada ya tukio lisilo la kawaida katika sherehe za kuadhimisha miaka 50 ya mtangazaji mkongwe wa Kenya, Fred Obachi Machoka.

Tukio hilo lilitokea katika hafla iliyofanyika Uwanja wa Michezo wa Ulinzi, jijini Nairobi, ambapo Koffi alionekana akifuatwa na kuombwa kuendelea na show baada ya kuondoka jukwaani bila sababu za msingi.

Video inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii inamwonesha Machoka akimkaribia mwanamuziki huyo, katika kile kinachoonekana kuwa jitihada za kumtuliza na kumshawishi asiache kutumbuiza.

Hata hivyo, mazungumzo yao yalionekana kuchukua mwelekeo usiokuwa wa kawaida baada ya Koffi kuonekana kutokuwa tayari kumsikiliza mtangazaji huyo. Katika sehemu moja ya video hiyo, mwanamuziki huyo anaonekana kumsukuma Machoka huku akijaribu kuzungumza naye.

Tukio hilo fupi limeibua hisia tofauti miongoni mwa Wakenya, huku baadhi wakieleza kutoridhishwa na kilichotokea na wengine wakitaka umma kusubiri maelezo zaidi kabla ya kutoa hukumu.

Hadi sasa, sababu iliyomfanya Koffi kuondoka jukwaani haijafahamika. Mwanamuziki huyo wala Machoka hawajatoa maelezo ya hadharani kuhusu kilichosababisha mvutano huo.

Mwezi Julai mwaka huo, mwanamuziki huyo alikabiliwa na ukosoaji mkubwa baada ya kusambaa kwa video iliyomwonesha akimpiga teke mmoja wa wachezaji wake wa kike katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA).

Tukio hilo lilizua hasira miongoni mwa wananchi, huku wengi wakitaka mwanamuziki huyo awajibishwe kwa kitendo hicho.

Tukio lake la hivi karibuni limefungua tena mjadala kuhusu uhusiano wake na mashabiki wa Kenya na matarajio ya watazamaji kwa wasanii wa kimataifa wanaotumbuiza nchini humo.

Koffi alikumbana pia na malalamiko kutoka kwa baadhi ya mashabiki waliohudhuria tamasha lake mjini Kisumu mwezi Desemba 2024.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, baadhi ya mashabiki hawakuridhishwa na onyesho hilo baada ya mwanamuziki huyo kuonekana bila bendi yake kamili.
Koffi Olomidé ni miongoni mwa majina makubwa katika muziki wa rhumba na soukous kutoka Kongo. Kwa miongo kadhaa, amejijengea umaarufu kupitia nyimbo zake zilizopata mashabiki wengi katika maeneo mbalimbali ya Afrika, ikiwemo Afrika Mashariki.

Related Articles

Back to top button