Makonda kuchangia milioni 50 ujenzi wa uwanja Kisesa

MWANZA: WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, ameahidi kuchangia Sh milioni 50 kwa ajili ya ununuzi wa nyasi bandia zitakazotumika katika uwanja wa mpira wa miguu wa Kisesa, Wilaya ya Magu, mkoani Mwanza.
Makonda ametoa ahadi hiyo wakati akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Magu katika ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza, akiwapongeza viongozi wa mkoa huo kwa kuanzisha mashindano mbalimbali ya kijamii yanayohusisha ngoma za asili, uimbaji na mpira wa miguu.
Amesema mashindano hayo ni miongoni mwa njia zinazoweza kuimarisha mshikamano wa wananchi, kukuza vipaji na kuwapa vijana fursa ya kutumia muda wao katika shughuli zenye manufaa.
Akizungumzia mpango wa kuboresha miundombinu ya michezo, Makonda amewataka wananchi na viongozi wa halmashauri kushirikiana kuchangia ujenzi wa uwanja wa kisasa wenye nyasi bandia katika eneo la Kisesa.
“Kwenye halmashauri hii tuwe na uwanja mmoja wa nyasi Kisesa. Sasa mjichange mjenge uwanja wenye nyasi nzuri bandia. Kwa kuwa nimekuja nyumbani, mtafute na mimi nitawaongezea Sh milioni 50 ili muweze kujenga kiwanja cha kisasa,” amesema Makonda.
Katika hatua nyingine, Waziri huyo ameeleza wasiwasi wake kuhusu mmomonyoko wa maadili katika jamii, akisisitiza umuhimu wa kurejesha misingi ya upendo, heshima na uwajibikaji.
Amesema Wizara anayoisimamia ina kitengo maalumu cha maadili, huku akilaani vitendo vya ulawiti dhidi ya watoto, wizi na uvunjaji wa nyumba vinavyofanywa na baadhi ya wahalifu mitaani.
Makonda amewataka wananchi kuimarisha utamaduni wa kujali majirani, kuwaheshimu wazee pamoja na viongozi wa dini na kimila, akisisitiza kuwa tofauti za kijamii hazipaswi kuwa chanzo cha migogoro.
“Kuna watu hawapendi amani, hawafurahii kuona watu hawaulizani kabila, dini au kipato. Tukiwa na tofauti tuwafuate wazee wetu watusuluhishe na si kugombana,” amesema.
Ziara hiyo ya siku nne mkoani Mwanza inalenga kukagua na kuzindua miradi 14 ya maendeleo pamoja na kutoa fursa kwa Waziri Makonda kuzungumza na wananchi na kusikiliza masuala mbalimbali yanayowahusu.




