Filamu

Mwigizaji wa ‘Breaking Bad’ RJ Mitte afariki dunia

BROWNSVILLE: MWIGIZAJI wa Marekani RJ Mitte, aliyepata umaarufu mkubwa kupitia tamthilia ya televisheni ya ‘Breaking Bad,’ amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 34, kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na wawakilishi wake pamoja na mamlaka nchini Marekani.

Taarifa za kifo chake, kwa mujibu wa shirika la habari la Associated Press (AP), Cyndi Hinojosa, hakimu wa amani katika Kaunti ya Cameron, alisema alithibitisha kifo cha Mitte katika eneo la Brownsville, Texas.
Hata hivyo, hadi taarifa hizo zilipochapishwa, sababu ya kifo chake ilikuwa bado haijafahamika hadharani.

Mamlaka zilisema uchunguzi wa maiti ulipangwa kufanyika ili kusaidia kubaini taarifa zaidi kuhusu kifo hicho.

Mitte alijulikana zaidi kwa kuigiza nafasi ya Walter White Jr., mtoto wa Walter White, mhusika mkuu aliyeigizwa na Bryan Cranston katika tamthilia ya ‘Breaking Bad’.

Tamthilia hiyo, iliyokuwa ikioneshwa kuanzia mwaka 2008 hadi 2013, ilipata umaarufu mkubwa kimataifa kutokana na simulizi yake kuhusu mwalimu wa kemia aliyeingia katika biashara ya utengenezaji na usambazaji wa dawa za kulevya.

Katika tamthilia hiyo, Mitte aliigiza mhusika mwenye ulemavu wa kupooza kwa ubongo, hali inayojulikana kwa Kiingereza kama (cerebral palsy). Jambo hilo lilikuwa na uhusiano na maisha yake halisi, kwani naye alikuwa akiishi na hali hiyo tangu utotoni.

RJ Mitte aligundulika kuwa na cerebral palsy akiwa na umri wa miaka mitatu. Kupitia kazi yake ya uigizaji na shughuli zake za kijamii, alijitahidi kuongeza uelewa wa jamii kuhusu watu wenye ulemavu na umuhimu wa kuwapa nafasi sawa katika sekta ya burudani na maeneo mengine ya maisha.

Mbali na ‘Breaking Bad,’ alishiriki katika miradi mingine ya filamu na televisheni, ikiwemo ‘Switched at Birth, Guardians of Justice’ na filamu ya ‘Triumph’ ya mwaka 2021.

Pia alihusika katika shughuli za utetezi wa haki za watu wenye ulemavu, akishirikiana na mashirika yaliyokuwa yakihamasisha ushirikishwaji na kuboresha maisha ya watu wenye (cerebral palsy) na changamoto nyingine za kiafya.

Kabla ya taarifa za kifo chake kutolewa, Mitte alikuwa akiendelea na shughuli za kutangaza filamu yake mpya, ‘Talking to Strangers’, kulingana na taarifa zilizoripotiwa na vyombo vya habari vya burudani.

Kifo chake kimehitimisha maisha ya mwigizaji aliyefanikiwa kujenga jina katika tasnia ya burudani huku akitumia uzoefu wake binafsi kuhamasisha mjadala kuhusu ulemavu na usawa.

Related Articles

Back to top button