
DAR ES SALAAM: MSANII wa filamu nchini Tanzania, Zaiylissa, amefunguka kuhusu sababu zilizomfanya ajikute akipata ujauzito akiwa na umri wa miaka 17,
Ameeleza kuwa malezi ya wazazi wa zamani yalijikita zaidi katika kuwabana watoto badala ya kuwapa elimu ya uzazi na malezi.
Zaiylissa amesema kuwa alipokuwa akipata ujauzito wake wa kwanza, ilikuwa vigumu kwake kuelewa hali aliyokuwa nayo kutokana na kukosa elimu ya kutosha kuhusu masuala ya uzazi.
Ameeleza kuwa katika kipindi hicho, mdogo wake Amina alikuwa msaada mkubwa kwake, kwani ndiye aliyeenda kununua kipimo cha ujauzito katika duka la dawa, akamwelekeza namna ya kukitumia na baadaye kumweleza pia kuhusu uwezekano wa kutoa mimba, ingawa yeye hakulikubali wazo hilo.
Kwa mujibu wa Zaiylissa, baada ya kuthibitisha kuwa alikuwa mjamzito, aliamua kwenda kumweleza mama yake kuhusu hali hiyo.
Hata hivyo, taarifa hizo hazikupokelewa vizuri, kwani mama yake alikasirika sana kiasi cha kutowasiliana naye kwa takribani wiki moja ndani ya nyumba.
Akizungumzia uzoefu wake huo, Zaiylissa amesema wazazi wa zamani walikuwa na tabia ya kuwabana watoto kupita kiasi bila kuwapa elimu muhimu ya uzazi, jambo ambalo kwa maoni yake linaweza kuchangia watoto kuingia katika uzazi wa mapema.
“Nina miaka 27, nilizaa nikiwa na miaka 17. Watoto hawatakiwi kuwabana sana.
Mimi nilibana kiasi kwamba nilipopata tu uhuru, mimba hii hapa,” amesema Zaiylissa.
Kupitia kauli yake hiyo, Zaiylissa amesisitiza umuhimu wa wazazi kujenga mazingira ya mazungumzo na watoto wao kuhusu uzazi, badala ya kutegemea zaidi marufuku na ukali.
Elimu sahihi ya uzazi na mawasiliano mazuri kati ya wazazi na watoto vinaweza kuwasaidia vijana kufanya maamuzi yenye uelewa na uwajibikaji.




