USIKU wa manane kwenye barabara fulani, mwigizaji maarufu anayeitwa Armaan Kapoor (Vivan Bhatena) anapoteza udhibiti wa gari lake bila sababu ya msingi.
Inaonekana kama vile alikuwa anajaribu kukwepa kitu fulani na hivyo analipeleka gari lake
baharini. Inspekta Surjan Shekhawat (Aamir Khan) na msaidizi wake Devrath Kulkarni (Rajkummar Rao) wanaanza uchunguzi wa kifo cha Armaan.
Surjan anagundua kuwa usiku wa ajali hiyo Armaan alikuwa anasafiri na fedha nyingi ambazo hata hivyo zinatoweka baada ya ajali.
Armaan alikuwa anakwenda kumpatia fedha hizo Shashi (Subrat Dutta) ambaye alimtishia kufichua siri yake na rafiki yake Sanjay Kejriwal (Suhaas Ahuja) ya miaka mitatu nyuma.
Sasa unaanza mchezo wa wajanja wa mjini kutapeliana. Shashi anaondoka na fedha za Armaan huku rafiki wa Shashi anayeitwa Tehmur (Nawazuddin Siddiqui) akiiba laini ya simu ya zamani ya Shashi.
Shashi anamtisha Sanjay akitaka ampatie fedha. Sanjay anakodi majambazi ambao
wanamuua Shashi. Rafiki wa Shashi, Tehmur anaitumia laini ya simu ya Shashi kumtisha Sanjay kwa mauaji ya Shashi.
Katika usiku mmoja, Inspekta Surjan anapendekezwa kuandamana na mwanadada Rosie (Kareena Kapoor), anakataa lakini anamwomba Rosie kumpa taarifa juu ya anachokifahamu.
Ndipo anagundua kuwepo kwa uhusiano wa Shashi katika kesi hiyo. Katika uchunguzi wao,
Polisi wanaupata mwili wa Shashi, fedha na DVD yenye video za CCTV zinazomhusu
Armaan na rafiki zake wakati wakiondoka eneo la hotelini wakiwa wameambatana na msichana mmoja.
Hapo sasa Inspekta Surjan anaanza uchunguzi wake karibu na hoteli hiyo. Mwanadada Rosie anamchukua Inspekta Surjan hadi mahali fulani pa ukimya sana na kumsimulia kuwa miaka mitatu iliyopita alichukuliwa na Armaan na rafiki zake, Sanjay na Nikhil (Prashant
Prakash).
Hata hivyo, haelezi chochote zaidi. Inspekta Surjan anaamua kumtafuta Nikhil lakini
anagundua kwamba ubongo wa Nikhil umeharibika baada ya tukio hilo na hivyo hawezi
kuwa msaada kwake.
Tehmur anauawa na wakora wawili waliokodiwa na Sanjay. Mmoja wa wakora hao anakamatwa na Polisi na anaeleza kila kitu anachokijua.
Inspekta Surjan anamkamata Sanjay, na baada ya kibano anakiri kuwa miaka mitatu iliyopita, yeye, Armaan na Nikhil walisherehekea siku ya kuzaliwa kwa Nikhil. Waliondoka katika hoteli moja wakiwa na msichana mmoja.
Walipokuwa njiani, Nikhil alianza kufanya mapenzi na msichana huyo katika kiti cha
nyuma ndani ya gari. Mlango wa gari ulifunguliwa kwa bahati mbaya, ukawatupa wote
nje ya gari barabarani, yaani Nikhil na msichana huyo na kuanguka barabarani.
Wote wawili waliumia sana. Armaan na Sanjay walimchukua Nikhil na kumkimbiza
hospitali lakini kwa kuwa waliogopa kashfa, wakaamua kumwacha yule msichana pale pale barabarani.
Hata hivyo, Sanjay alimpigia simu Shashi kumwomba amsaidie yule msichana. Shashi aliwaambia kuwa msichana huyo amekufa na alikuwa na picha zao wote watatu wakati wakiondoka na kumwacha hapo barabarani.
Tangu wakati huo, Shashi alikuwa akiwatisha kwa lengo la kutaka kujipatia fedha kutoka
kwao ili asivujishe siri yao. Inspekta Surjan anachunguza kwa umakini video hiyo na kugundua kuwa msichana aliyekufa ni Rosie.
Anampeleka Sanjay hadi kituo cha Polisi, na wanapofika eneo lile lile ambalo Armaan alipata ajali na gari kutumbukia baharini, Inspekta Surjan na Sanjay wanamwona Rosie akiwa kasimama mbele yao.
Sanjay anayumba na gari linaingia baharini. Sanjay anakufa, Inspekta Surjan anatoka kwa kuokolewa na Rosie mwenyewe.
Mkuu wa Inspekta Surjan anamshauri askari huyo kutoandika taarifa za hadithi yake ya ajabu kwenye kesi hiyo, na hivyo, Inspekta Surjan anaandika ripoti kwamba kifo cha Armaan ilikuwa ni ajali kama zilivyo ajali zingine… Talaash: The Answer Lies Within ni filamu iliyoandikwa na kuongozwa na Reema Kagti, ilitolewa Novemba 30, 2012, stori yake ikiwa imejikita kwenye simulizi za kutisha.
Ni filamu ya dakika 139 iliyofanikiwa kujikusanyia zaidi ya dola milioni 25 za Marekani duniani kote na kuwa moja ya filamu za India zilizoingiza mapato makubwa mwaka 2012.
0685 666964 au bjhiluka@yahoo.com