Ligi Ya Wanawake

Twiga Stars iko tayari kuivaa Botswana leo

DAR ES SALAAM: TIMU ya taifa ya wanawake Twiga Stars leo itashuka dimbani kuivaa Botswana katika mchezo wa mkondo pili huku Kocha Mkuu Bakari Shime, akisema maandalizi ya kikosi chake yamejikita kulinda ushindi uliopita na kupata matokeo mazuri.

Shime amesema matokeo ya mchezo wa kwanza yamepita na sasa kikosi chake kinapaswa kuhakikisha kinapambana mwanzo mwisho katika mchezo mwingine mpya, utakaochezwa leo saa 10:00 jioni katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.

Amesema kipaumbele cha benchi la ufundi kimekuwa kuhakikisha wachezaji wanapata muda wa kutosha wa kurejesha nguvu baada ya safari ili wawe tayari kukabiliana na Botswana na hilo tayari wamelitimiza.

Ameongeza kuwa katika muda uliobaki kabla ya mchezo, benchi la ufundi litawakumbusha wachezaji mambo muhimu ya mchezo wa kwanza, likisisitiza mbinu za kujilinda, kushambulia na kuzuia wapinzani ili kuhakikisha wanatumia vizuri faida ya bao moja waliyoipata ugenini.

Shime amesema anaamini wachezaji wataweza kukumbuka maelekezo ya kiufundi na kuyatekeleza katika mchezo huo muhimu, huku akisisitiza umuhimu wa kucheza kwa nidhamu ili kupata matokeo yatakayoiwezesha Twiga Stars kusonga mbele katika mbio za kufuzu Olimpiki 2028.

 

Related Articles

Back to top button