Mwambusi alilia uzembe wa wachezaji

DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa Coastal Union, Juma Mwambusi, ameonesha masikitiko yake kufuatia uzembe uliofanywa na wachezaji wake, ambao umewagharimu nafasi ya kusonga mbele katika Kombe la Shirikisho la CRDB (FA).
Timu yake iliondolewa kwenye mashindano hayo baada ya kupokea kichapo cha mabao 3-1 dhidi ya Yanga, katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya mchezo, Mwambusi alisema wachezaji wake walikosa umakini, hasa katika kipindi cha kwanza, na kufanya makosa yaliyoigharimu timu kwa kufungwa mabao mawili mapema.
“Wachezaji wangu hawakuwa makini. Tunapocheza dhidi ya Yanga, ambayo ina ubora mkubwa, ni lazima tuwe waangalifu na kuheshimu mchezo.
Tulifanikiwa kutengeneza nafasi na kupata bao la kwanza, nikaona tunaweza kusawazisha, lakini tukafanya uzembe na tukafungwa bao la tatu,” amesema.
Mwambusi amesema wanayachukua matokeo hayo kama funzo na sasa wanarejea mazoezini kwa maandalizi ya michezo ijayo ya Ligi Kuu Tanzania Bara.