JKT Tanzania yautaka Ubingwa wa Shirikisho

DAR ES SALAAM:KATIKA safari yao ya kuelekea mafanikio makubwa, Klabu ya JKT Tanzania imeweka wazi dhamira yao ya kutinga fainali na hatimaye kutwaa ubingwa wa michuano ya Kombe la Shirikisho la CRDB.
Haya yamebainishwa na Msemaji wa timu hiyo, Masau Bwire, ambaye amesema kuwa timu hiyo ipo tayari kwa hatua zinazofuata, ikiwemo nusu fainali dhidi ya mabingwa watetezi, Yanga SC.
JKT Tanzania walifuzu hatua ya nusu fainali baada ya kuichapa Pamba Jiji FC, na sasa wanajipanga kwa pambano kali dhidi ya Yanga kati ya Mei 16 hadi 18.
Kwa mujibu wa Bwire, lengo lao si kufika tu nusu fainali, bali kwenda mbali zaidi kwa kutinga fainali, kutwaa taji, na hatimaye kuwakilisha taifa kwenye michuano ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
“Hatutaki tu kushiriki, tunataka kufanikisha ndoto ya kuwa mabingwa na kutangaza jina la JKT Tanzania kimataifa, uongozi wa juu wa JKT umejipanga vyema kuhakikisha timu inapata kila inachohitaji kufanikisha malengo hayo, ikiwa ni pamoja na maandalizi bora na hamasa kubwa kwa wachezaji.
Tofauti na baadhi ya timu ambazo zimejikuta zikipata changamoto za kifedha hadi kushindwa kusafiri kwa wakati kwenye mashindano ya kimataifa, Bwire amesema JKT Tanzania wamejipanga kuhakikisha hali hiyo haitokei.
“Ni aibu kwa timu kushindwa hata kupata nauli ya kusafiri, lakini sisi tuna uhakika huo hautakuwa changamoto. Uongozi umejipanga kikamilifu kuhakikisha timu inasafiri mapema na kwa maandalizi mazuri kabla ya mechi yoyote ya kimataifa,” amesisitiza.