Ligi Kuu

Mubiru wa Azam anautaka ubingwa wa ligi

DAR ES SALAAM: WINGA wa Azam FC, Hassan Mubiru ameeleza wazi kuwa msimu huu amedhamiria kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara akiwa na timu hiyo.

Mubiru aliyetua Azam msimu huu akitokea SC Villa ya Uganda amesema anafahamu ugumu uliopo katika kukamilisha hilo ndiyo maana kila mechi kwao ni fainali.

“Kwanza ni heshima kwangu kuvaa nembo ya Azam, ina historia na ni klabu kubwa, nasikia furaha kujiunga na klabu hii nzuri na ninatarajia kufanya vizuri nikiwa hapa.

“Nashukuru Mungu tunapata matokeo japo ni ngumu kupata ushindi kila mchezo, na malengo yetu msimu huu ni kuchukua kombe. Nataka kuchukua kombe nikiwa na Azam hivyo kila mechi kwetu ni fainali,” alisema Mubiru raia wa Uganda.

Aidha, nyota huyo amebainisha kuwa kufunga bao na kuwa mchezaji bora katika mechi yao ya mwisho dhidi ya Namungo waliyoshinda mabao 2-0, imemuongezea ari na kumfungulia njia ya kutupia zaidi msimu huu.

“Ni kweli lile bao limenifungulia njia nzuri msimu huu na kunipa ujasiri wa kuendelea kufanya vizuri nikiwa hapa na kusaidia kutimiza malengo ya Azam,” alihitimisha Mubiru.

Azam ambayo ilitwaa ubingwa mara ya kwanza na ya mwisho msimu wa 2013-14, kwenye msimamo inashika nafasi ya tatu kwa pointi 14 baada ya michezo sita, nyuma ya Yanga na Simba zenye pointi 15 baada ya kila moja kucheza mechi tano.

Related Articles

Back to top button