Spice Girls wazua zogo la uwezekano wa kuungana kwao upya

LONDON: KUNDI maarufu la muziki wa pop kutoka Uingereza, Spice Girls, limewaacha mashabiki wake katika sintofahamu baada ya kutoa ujumbe mfupi wa siri unaoashiria uwezekano wa kutangaza jambo kubwa.
Spice Girls, ambalo lilipata umaarufu mkubwa duniani katika miaka ya 1990, linahusisha wanamuziki akiwemo mke wa aliyekuwa mchezaji wa soka Manchester United na Real Madrid Davidi Beckam, Victoria Beckham, Melanie Brown, Melanie Chisholm, Emma Bunton na Geri Halliwell.
Ujumbe huo uliambatana na tarehe 10.09.2026 pamoja na muda wa saa 2:00pm, hali iliyochochea mijadala miongoni mwa mashabiki na wafuasi wa kundi hilo duniani.
Taarifa hiyo imeleta matarajio kwamba Spice Girls huenda likatangaza muungano mpya au tukio maalumu linalohusishwa na historia ya kundi hilo. Mashabiki wamekuwa wakisubiri kwa muda mrefu kuona tena wanamuziki wa kundi hilo wakikutana kwenye jukwaa moja, hivyo ujumbe wa tarehe na muda maalumu umechukuliwa kama ishara ya kurudiana kwao.
Kundi hilo lilitikisa tasnia ya muziki wa pop kupitia nyimbo zake zilizofanikiwa kimataifa na likawa moja ya makundi ya kike yenye ushawishi mkubwa katika historia ya muziki wa pop.
Katika miaka ya hivi karibuni, wanachama wa Spice Girls wamekuwa wakifanya shughuli zao binafsi, huku kukiwa na matukio machache ya kuwaona pamoja. Miongoni mwa matukio yaliyowahi kuvuta hisia za watu ni ziara yao ya mwaka 2019 iliyowakutanisha baadhi ya wanachama wa kundi hilo jukwaani, ingawa Victoria Beckham hakushiriki katika ziara hiyo.
Ujumbe mpya umetokea wakati mashabiki wakiendelea kuzungumzia uwezekano wa kundi hilo kurejea pamoja, hasa katika kipindi ambacho muziki wa miaka ya zamani umeendelea kupata umaarufu kupitia mitandao ya kijamii na majukwaa ya kidijitali. Hata hivyo, hadi muda wa taarifa hii, bado haijawekwa wazi rasmi ikiwa tangazo hilo litahusu reunion, muziki mpya, tamasha au tukio jingine maalumu.
Kwa sasa, macho na masikio ya mashabiki wa Spice Girls yako kwenye muda uliotajwa wa 2:00 usiku wa leo wakisubiri kujua siri iliyofichwa nyuma ya ujumbe huo. Endapo itathibitika kuwa ni muunganiko mpya hatua hiyo inaweza kuwa moja ya habari kubwa kwa mashabiki wa muziki wa pop duniani.




