‘Tunataka Selemani awe na furaha na kazi yake’

DAR ES SALAAM: MENEJA wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ali Kamwe, amesema klabu hiyo haitamlazimisha mshambuliaji wake mpya, Selemani Mwalimu, kuonesha ushabiki wa Yanga, akisisitiza kuwa alisajiliwa kama mchezaji wa kulinda na kuendeleza taaluma yake.
Kamwe amesema Yanga imeamua kumkaribisha Mwalimu kwa utamaduni wake kwa kumuonesha upendo na kumfanya ajisikie sehemu ya familia ya klabu hiyo, baada ya kujiunga na timu hiyo akitokea klabu pinzani.
Amesema uhamisho wa mchezaji kutoka timu moja kwenda nyingine unaweza kuleta hisia tofauti kwa mashabiki wa klabu aliyotoka, hivyo ni jukumu la mashabiki wa Yanga kumpokea na kumpa mazingira yatakayomsaidia kuondokana na presha hiyo.
“Tumemsajili Sele kama mchezaji mwenye uwezo anayeheshimu kazi yake. Anatakiwa apate nafasi atupambanie acheze,” amesema Kamwe.
Amesema furaha haiwezi kulazimishwa kwa mchezaji, hivyo Yanga inataka Mwalimu awe na furaha katika kazi yake, aheshimu majukumu yake na afanye kile alichosajiliwa kufanya uwanjani.
Kamwe amesema klabu hiyo imeandaa mpango maalumu wa kumpokea Mwalimu katika mchezo ujao, akitaka mashabiki wamuonyeshe utamaduni wa Yanga na mapenzi waliyonayo kwa wachezaji wao.
Ameongeza kuwa jukumu la mashabiki ni kumpa mchezaji huyo upendo na kumuamini, huku jukumu la Mwalimu likiwa ni kulipa kwa kiwango kizuri uwanjani na kuipambania Yanga.
Kamwe amesema uhamisho wa wachezaji ni sehemu ya kawaida ya soka, hivyo mashabiki wanapaswa kuelewa kuwa mchezaji anaweza kuwa upande mmoja leo na kesho akawa sehemu ya timu nyingine.




