Kamwe akiri ugumu wa Kariakoo Derby

DAR ES SALAAM: OFISA Habari wa Yanga, Ali Kamwe, amesema kuwa mchezo wa Kariakoo Derby dhidi ya watani wao wa jadi, Simba, utakuwa mgumu zaidi kutokana na historia ya ushindi wa mara nne mfululizo wa Yanga dhidi ya wapinzani wao.
Kamwe amesema kuwa Simba wataingia katika mchezo huo kwa dhamira ya kufuta rekodi mbaya ya kufungwa mara nne mfululizo na kutafuta ushindi.
Mchezo huo, ambao utapigwa Jumamosi, Machi 8, katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, utaikutanisha Yanga kama wenyeji dhidi ya Simba katika pambano la kukata na shoka.
“Tunafahamu umuhimu na thamani ya kushinda Kariakoo Derby. Maandalizi yameshaanza na wachezaji wako kambini kwa ajili ya mchezo huu.
Hata hivyo, tunaelewa kuwa rekodi yetu ya kushinda mara nne inafanya mchezo huu kuwa mgumu zaidi kwa sababu wapinzani wetu wanataka kufuta uteja na kulipa kisasi,” amesema Kamwe.
Hata hivyo, Kamwe hakubaliani na maoni ya baadhi ya watu wanaodai kuwa matokeo ya mchezo huo yataamua bingwa wa ligi msimu huu.
“Sikubaliani na wanaodai kuwa mchezo huu utaamua ubingwa. Baada ya mechi dhidi ya Simba, bado tuna michezo saba mbele yetu, ambayo inajumuisha alama 21 za kugombania.
Kushinda Kariakoo Derby ni muhimu, lakini si kipimo cha ubingwa. Hatutaki kushinda Derby kisha kupoteza michezo mingine, kwani bingwa hupatikana kwa kuvuna alama nyingi mwishoni mwa msimu,” ameongeza Kamwe.
Macho na masikio sasa yanaelekezwa kwenye Uwanja wa Mkapa, huku mashabiki wa pande zote mbili wakisubiri kwa hamu kuona nani ataibuka mbabe katika mchezo huu wa kihistoria.