Moalin: Awesu ni mtu na nusu!

DAR ES SALAAM: KOCHA Mkuu wa KMC FC, Abdulhamid Moalin ameweka wazi bado ataendelea kumkumbuka aliyekuwa kiungo wa timu hiyo, Awesu Awesu, aliyejiunga na Simba kwa msimu huu wa 2024/25.
Amesema licha ya kumhusudu mchezaji huyo anamtakia kheri lakini ataendelea kumkumbuka kutokana na uwezo wake na kusaidia timu hiyo msimu uliopita kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.
“Awesu ni mchezaji mzuri na sasa amepata timu nyingine, atakuwa katika kumbukumbu zangu licha ya kuwepo kwa vijana wengine, tutakaowatengeneza kuja kuziba nafasi yake,” amesema kocha huyo na kuweka wazi mipango yao ya mchezo wa kesho dhidi ya Coastal Union.
Kuelekea mchezo huo, Moalin amesema wamefanya maandalizi mazuri na wanahitaji kuanza vema kampeni yao ya kusaka ushindi katika mchezo wa kwanza wa ligi dhidi ya Coastal Union.
Moalin amesema amewaona ubora na madhaifu ya wapinzani wao hao na wataingia kwa tahadhari kubwa katika mchezo huo kuhakikisha wanatumia vema uwanja wa nyumbani.
Naye nyota wa KMC, Hans Masoud ameweka wazi kuwa mcheza kwao hutunzwa na watapambana kutafuta matokeo chanya katika mchezo wa kwanza wa ligi dhidi ya Coastal Union.
“Msimu uliopita tuliambulia pointi mbili dhidi ya Coastal Union, lakini safari hii tunahitaji pointi tatu za nyumbani na vizuri mechi yetu ya kwanza tunaanza nyumbani, tena kwenye uwanja wa KMC,” amesema Hans.