“BASATA hakuna upendeleo wasanii wote ni sawa”

DAR ES SALAAM: Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Kedmon Mapana, amesisitiza kuwa baraza hilo halina upendeleo na linafanya kazi na wasanii wote kwa usawa, bila kujali ukubwa wao katika tasnia.
Akizungumza wakati wa mafunzo ya uzingatiaji wa maadili kwa wasanii na waandishi wa habari, Mapana alieleza kuwa kila msanii anayewasilisha kazi yake kwa BASATA hupitia mchakato wa tathmini sawa bila upendeleo wowote.
“Msanii Diamond Platnumz alinitumia wimbo wake kwa ajili ya kupitia na kupewa daraja. Wimbo huo ulipewa daraja X, ikimaanisha kuwa ulikuwa na sehemu zilizohitaji marekebisho. Diamond alikubali na kufanya marekebisho hayo. Huu ni utaratibu wa kawaida kwa kila msanii,” amesema Mapana.
Amesema kuwa lengo la BASATA si kupingana na wasanii kuhusu masuala ya maadili, bali kushirikiana nao kwa karibu ili kuhakikisha kazi zao zinafuata viwango vilivyowekwa.
“Hatupendi kuwa na migongano na wasanii kuhusu maadili. Tunapenda ushirikiano, ndiyo maana tunaandaa mafunzo kama haya ili kuwaelimisha na kuwaweka karibu nasi. BASATA ni sehemu ya wasanii, na wasanii ndio wanaounda BASATA,” ameongeza Mapana.