Mjerumani apewa England

KOCHA wa zamani wa Bayern Munich, Chelsea, PSG na Borussia Dortmund, Thomas Tuchel ametangazwa kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya England.
Chama cha Soka nchini England ( FA ) kimetoa taarifa hiyo na kutangaza kwamba bingwa huyo aliyewahi kubeba UEFA atasaidiwa na kocha wa Kiingereza Anthony Barry.
Tuchel anarejea kufanya kazi nchini humo baada ya kufanya kazi akiwa na Chelsea na kuisaidia kutwaa taji la Ulaya pamoja Ubingwa wa Dunia wa Vilabu. Sambamba na hilo, Tuchel alipigiwa kura kama kocha bora wa UEFA na FIFA wa mwaka 2021 kutokana na mafanikio yake klabuni Chelsea.
Baada ya England kumfuta kazi Gareth Southgate, timu hiyo inanolewa na kocha wa mpito Lee Carsley ambaye ataendelea na kazi hiyo mpaka Tuchel atakapoanza kazi rasmi mnamo Januari mosi 2025.
Tuchel na Barry wanarudi kufanya kazi kwa pamoja baada ya kufanya hivyo wakiwa Chelsea na Bayern ambako kwa pamoja walifanikiwa kutwaa mataji manne.
Thomas Tuchel alisema: “Ninajivunia sana kupewa heshima ya kuongoza timu ya England. Nimekuwa na uhusiano wa kibinafsi na mchezo huu nchini humu kwa muda mrefu, na umenipa nyakati za kipekee tayari. Kuwa na nafasi ya kuiwakilisha England ni fursa kubwa, na nafasi ya kufanya kazi na kundi hili la wachezaji mahiri na wenye vipaji ni jambo la kusisimua sana.”
Naye kocha msaidizi Anthony Barry aliongeza: “Kwa kila Mwingereza aliye kwenye soka, kufanya kazi na timu ya taifa ni kilele cha mafanikio, na sikusita nilipoombwa na Thomas kujiunga naye tena. Najua jinsi St. George’s Park ilivyo mahali pazuri na faida kubwa inayoipa timu zetu za England, pamoja na msaada inaowapa makocha.
“Kikosi hiki kina vipaji vikubwa na kimefanya mengi kuleta umoja nchini. Natarajia kukutana nao na kufanya kazi nao katika mradi huu wa kusisimua.”
Akiwa na Chelsea kwenye EPL, Tuchel aliiongoza timu hiyo katika michezo 63,akishinda 35,sare 17 na kupoteza 11. Timu hiyo ilifunga mabao 109 na kufungwa mabao 55.