Michuano ya kanda ya Karate kufanyika Iringa

DAR ES SALAAM: SHIRIKISHO la Karate Tanzania limeandaa mashindano ya Taifa ya kanda yatakayofanyika Juni 28-29 katika kumbi za Chuo Kikuu RUCU mkoani Iringa.
Kwa mujibu wa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Karate Tanzania, Sensei Said Kiswabi mikoa zaidi ya 10 inatarajia kuoneshana kazi.
Kiswabi amesema mashindano hayo yatashirikisha wachezaji zaidi ya 100 wa nafasi ya mchezaji mmoja mmoja na timu katika uzito tofauti .
Aidha, ametaja baadhi ya mikoa itakayoshiriki ni pamoja na Shinyanga, Iringa, Dar es Salaam ambayo inashirikisha mikoa minne, Zanzibar, Dodoma na Singida.
Mmoja wa wachezaji watakaoshiriki mashindano hayo, Juma Mustafa amesema amejiandaa vilivyo kwa ajili ya mashindano hayo na kutoa wito kwa wadau mbalimbali kujitokeza na kujionea vipaji vya michezo.




