Nyumbani

WanaSimba Amkeni, hiyo ndoto ni mbaya

Kwenye maisha siku zote kuna kupanda na kushuka, wengi tunachukia kushuka na kufanya sherehe pale tunapopanda.

Tunasahau maisha ni kama pande mbili za sarafu, kila upande humtegemea mwenzake ili kukamilisha uwepo wa sarafu hiyo.

Inafikirisha sana wale wanaotushangilia tukiwa kwenye kilele cha mafanikio ndio hawa wanaotuzomea, kutudhihaki na kutuombea mabaya pindi tunapokuwa kwenye anguko(kushuka).

Nimefuatilia vyema kile kinachoendelea kwa Golikipa wa Simba Aishi Manula, ni rahisi kusema Simba wanalazimisha kumtoa moyoni mtu wanaempenda sana, wanalazimisha kuvunja penzi kwa kisingizio cha chumvi kuzidi kwenye chakula?.

Niaamini Wanasimba wapo ndotoni na hii ndoto haipaswi kuwa kweli ikatishwe haraka!

Simba amkeni Manula hastahili hata kidogo anayoyapitia kwasasa, mwanadamu ameumbiwa mapito huenda na yeye yupo katika wakati huo, hivi ni kweli leo hii chapisho la Manula pale Instagram limejaa matusi yenu? amkeni wanasimba sio sawa.

Ni ngumu sana kuyasahau makubwa aliyoyafanya Manula kwa misimu yote aliyokuwa Simba kwa matukio machache na ya muda mfupi tena yasiyokuwa na uhakika.

Mjenzi aliyeshiriki kuijenga ngome imara ya mnyama Afrika leo hii anaonekana msaliti? tena katika mazingira ambayo kila mtu anafahamu kipa huyu alikuwa majeruhi? na bado alikuwa akijitafuta kurudi tena, hizi ni hatua kwenye maisha kuna kupanda na kushuka.

Manula aliyeshinda tuzo ya golikipa bora wa msimu mara tano mfululizo hastahili hata punje ya anayofanyiwa kwasasa, ushabiki wetu kwa timu zetu usitusahaulishe tukavunja heshima za watu.

Nyakati zinakuja, nyakati zinapita, tukumbuke kuweka akiba ya maneno, ukweli ni kwamba kama ubora wake hauwaridhishi hakuna haja ya kumdhihaki au kumshtumu tuupe muda nafasi.

Ninafahamu somo la uvumilivu katika mazingira yetu ya soka ni gumu mno lakini tuzikatae hisia mbaya zilizo kifuani mwetu zikitaka tuwavunjie heshima mashujaa wetu, ukweli ni kwamba ni ngumu kujivunia ukubwa huu klabu inayotamba nayo kwasasa Afrika bila jina la huyu kijana wa Morogoro.

Basi apewe maua yake na anapokosea aambiwe kama wanavyoambiwa wengine ila matusi dhihaka na kashfa zinavunja patano la mapenzi ya kweli baina yenu.

Related Articles

Back to top button