Nyumbani

Michezo ni sekta inayopewa kipaumbele na serikali

IRINGA: SERIKALI imeahidi kuendelea kuipa kipaumbele sekta ya michezo nchini kutokana na mchango wake mkubwa katika maendeleo ya vijana, uchumi wa taifa na kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia mashindano mbalimbali.

Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma, wakati akifunga mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma Tanzania kwa Shule za Msingi (UMITASHUMTA) mwaka 2026 yaliyofanyika mkoani Iringa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwinjuma amesema serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Dk Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika maendeleo ya michezo kwa kutambua nafasi yake katika kukuza vipaji, kuimarisha afya za wananchi na kutoa ajira kwa maelfu ya vijana.

Amesema Rais Samia ameonesha dhamira ya dhati ya kuendeleza sekta za michezo, sanaa na utamaduni kwa kuweka mazingira rafiki yanayowawezesha vijana kutumia vipaji vyao kujiletea maendeleo binafsi na kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi.

“Serikali inaamini michezo si burudani pekee, bali ni nyenzo muhimu ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Ndiyo maana tutaendelea kuwekeza katika miundombinu ya michezo, kuendeleza mashindano mbalimbali na kuhakikisha vipaji vya vijana vinatambuliwa na kuendelezwa,” amesema Mwinjuma.

Ameeleza kuwa juhudi zinazofanywa na serikali zimeanza kuzaa matunda, ambapo vijana wengi wamefanikiwa kupata ajira na kipato kupitia michezo mbalimbali, huku wengine wakipata fursa za kuiwakilisha Tanzania katika timu za taifa na mashindano ya kimataifa.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa mashindano ya UMITASHUMTA katika kutambua na kukuza vipaji vya watoto tangu wakiwa katika ngazi za elimu ya msingi, akibainisha kuwa baadhi ya wanamichezo maarufu nchini wamepitia mashindano hayo kabla ya kufikia mafanikio makubwa.

Ametoa wito kwa walimu, wazazi na wadau wa michezo kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuibua na kuendeleza vipaji vya watoto ili kujenga kizazi chenye uwezo wa kushindana katika medani mbalimbali za michezo duniani.

Related Articles

Back to top button