Simba, Yanga, Azam kazi kwenu

DAR ES SALAAM: SIKU moja baada ya mabadiliko ya Kanuni za usajili uliofanywa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuongeza muda wa klabu katika usajili, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi kuu Tanzania (TPLB), Almas Kasogo amesema wamepokea taarifa hizo sasa jukumu lipo kwa klabu za Tanzania kutumia nafasi hiyo.
Kasongo amesema kufungua dirisha kipindi cha miezi miwili hii inatoa nafasi kwa klabu zinazoenda kushiriki kombe la Dunia la Klabu kutoa nafasi ya kuimarisha timu zao hasa kwa timu za Afrika zilizopata nafasi ya kwenda kushiriki michuano hiyo.
“Itategemea na mahitaji ya wadau wetu, Bodi na TFF ni mali za klabu pale wanaona kuna haja ya kutumia hiyo fursa ya CAF basi tutakaa na kuangalia, wadau na wenye mpira ni klabu wakihitaji basi chombo hatuna pingamizi,” amesema.
Kauli Kasongo ni baada ya CAF kutoa taarifa juu ya kubadilisha kanuni za usajili wa wachezaji za Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho la CAF, kuruhusu klabu kupata muda mrefu wa kusajili wachezaji kwa ajili ya mashindano hayo ndani ya msimu huu wa Soka.
Marekebisho ya Kanuni hizo sasa zinafanana na UEFA Champions League na Kanuni za Usajili wa Wachezaji wa UEFA Europa League, yatachangia Ligi ya Mabingwa wa CAF na Kombe la Shirikisho la CAF kuwa ya kuvutia na yenye mvuto kwa mashabiki wa soka,
Mabadiliko haya yanaweza pia kuboresha ubora wa klabu za Afrika zinazoshiriki Kombe la Dunia la Klabu la FIFA 2025 litakalofanyika Marekani mnamo Juni-Julai 2025, Kamati ya CAF ilichukua azimio la kuongeza muda wa mwisho wa Usajili wa Wachezaji wa Ligi ya Mabingwa ya CAF na Kombe la Shirikisho la CAF hadi 28 Februari 2025.