Dar City yaichapa Srelio, Mlimani nayo yaibuka

DAR ES SALAAM:TIMU ya Dar City imeendeleza ushindani katika Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam baada ya kuichapa Srelio kwa pointi 95-42 katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Don Bosco, Upanga jana usiku.
Dar City ilianza mchezo huo kwa kasi, ikitawala mchezo katika robo ya kwanza na kuongoza kwa pointi 20-10 dhidi ya Srelio.
Katika robo ya pili, Dar City iliendelea kushikilia mchezo na kuongeza pointi zake hadi kufikisha 44, huku Srelio ikiwa na pointi 30 wakati timu hizo zikienda mapumziko.
Baada ya mapumziko, Dar City iliendelea kuonesha ubora wake na kufikisha pointi 69 dhidi ya 38 za Srelio mwishoni mwa robo ya tatu.
Robo ya nne haikubadili mwelekeo wa mchezo huo, kwani Dar City iliendelea kutawala na hatimaye kumaliza kwa ushindi mkubwa wa pointi 95-42.
Katika mchezo mwingine Mlimani iliibuka na ushindi wa pointi 76-59 dhidi ya Chui katika mchezo mwingine uliochezwa Don Bosco.
Pia, Jeshi Stars ilipata ushindi wa pointi 60-40 dhidi ya Vijana Queens, huku UDSM Outsiders ikiibuka na ushindi wa pointi 46-31 dhidi ya JKT.




