Ligi KuuNyumbani

JKT Tanzania kuingia sokoni dirisha dogo

KOCHA Mkuu wa JKT Tanzania, Malale Hamsini amesema ana mpango wa kusajili wachezaji wawili kwenye dirisha dogo ili kikosi chake kizidi kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.

Akizungumza na gazeti la HabariLEO, Malale amesema nafasi ambazo amekusudia kuziboresha ni ushambuliaji na kiungo ambazo amebaini zina mapungufu.

“Tumecheza mechi tisa hatupo nafasi mbaya lakini ushindani ni mkubwa, tunapaswa kuwa na kikosi imara chenye wachezaji wenye uwezo na uzoefu ambao watatufikisha kwenye malengo yetu,” amesema Malale.

Kocha huyo amesema kuumia kwa kiungo Hassan Dilunga na safu yake ya ushambuliaji kukosa makali kama ilivyokuwa msimu uliopita kwenye Championship ndio kumemlazimu kurudi sokoni kusajili nyota wapya ili kuongeza nguvu kabla ya kuanza mzunguko wa pili.

Amesema anaridhishwa na viwango vya wachezaji waliopo na upambanaji wao lakini kutokana na ugumu wa ligi msimu huu anahitaji kuwa na kikosi imara ambacho hakitegemei mchezaji mmoja.

JKT Tanzania ipo nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikikusanya pointi 14 katika michezo tisa iliyocheza hadi sasa.

Related Articles

Back to top button