Nyumbani

Barker: Bado kuna kazi dirisha la usajili

DAR ES SALAAM:KOCHA wa Simba, Steven Barker, amesema bado kuna kazi ya kufanya ndani ya kikosi chake baada ya kupoteza dhidi ya Yanga, huku akiacha mlango wazi kwa klabu hiyo kufanya usajili zaidi kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili.

Simba ilipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Yanga katika mchezo wa Ngao ya Jamii, matokeo ambayo Barker amesema yamewapa picha ya maeneo wanayopaswa kuyafanyia kazi kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Barker amesema licha ya matokeo hayo, amevutiwa na namna wachezaji wake walivyojituma, lakini bado hawajafikia kiwango anachotaka.

“Bado tuna kazi ya kufanya. Wachezaji wameonesha kujituma na wamefanya kazi kwa bidii, lakini kwa sasa hatujafikia kiwango chetu bora. Nafikiri mchezo huu utatusaidia kufikia kiwango tunachohitaji,” amesema Barker.

Kocha huyo amesema Simba ilianza mchezo kwa kiwango kizuri na kutawala dakika 20 hadi 25 za mwanzo, lakini ikashindwa kutumia kipindi hicho kupata bao la kuongoza.

Barker amesema katika kipindi cha pili Simba ilikosa makali na mtiririko mzuri wa mashambulizi, hasa ilipofika katika eneo la mwisho la uwanja.

Barker pia ameeleza sababu ya kumpanga Elie Mpanzu kipindi cha pili, akisema mchezaji huyo aliwasili kambini akiwa amechelewa kutokana na changamoto za safari kuelekea Kigali, hivyo hawakutaka kumlazimisha kucheza dakika zote.

Akizungumzia usajili, Barker hakufunga milango ya Simba kuongeza wachezaji kabla ya dirisha la usajili kufungwa.

Huenda ndani ya siku mbili zilizobaki kabla ya kufungwa kwa dirisha Simba ikatangaza usajili mwingine kwani kumekuwa na tetesi juu ya wachezaji inaowahitaji.

 

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button