Mastaa

Jux Awajibu wanaoendesha kampeni ya ‘FreeJux’

MSANII wa Bongo Fleva, Juma Jux, amewajibu mashabiki na watumiaji wa mitandao ya kijamii wanaoendesha kampeni ya ‘FreeJux’, akisisitiza kuwa hana tatizo lolote katika ndoa yake na kwamba mabadiliko ya muonekano wake yanatokana na jitihada za kuishi maisha yenye afya zaidi.

Kampeni hiyo ilianza kushika kasi mitandaoni baada ya baadhi ya watu kubaini kuwa Jux amepungua uzito na kuhusisha hali hiyo na changamoto za ndoa yake na mkewe, Priscilla Jux.

Hata hivyo, baada ya Watanzania wengi kufurika katika ukurasa wa Instagram wa Priscilla na kuandika ujumbe wa #FreeJux, msanii huyo ameamua kuweka wazi msimamo wake kupitia Snapchat.

Katika video aliyochapisha, Jux alisema lengo lake ni kuboresha afya yake kwa kufuata mtindo bora wa maisha, jambo ambalo baadhi ya watu wameonekana kutolikubali.

“Nataka tu kuwa mwenye afya zaidi, lakini watu hawakubaliani na hilo,” alisema Jux katika video hiyo.

Baadaye aliongeza ujumbe mfupi uliowalenga wanaoendeleza kampeni hiyo akisema, “Don’t free me please,” akimaanisha kuwa hana haja ya kuokolewa kama ambavyo baadhi ya mashabiki wanavyodhani.

Kauli hiyo imezua mjadala mkubwa mitandaoni, huku wengine wakimuunga mkono na kueleza kuwa mabadiliko ya mwili yanaweza kutokana na mazoezi na mtindo wa maisha wenye afya, wakati wengine wakiendelea kutoa maoni yao kuhusu muonekano wake mpya.

Jux na Priscilla wameendelea kuonesha ukaribu wao kupitia machapisho mbalimbali ya mitandao ya kijamii, licha ya mjadala unaoendelea kuhusu kampeni ya #FreeJux.

Related Articles

Back to top button