Amani Josiah afichua mbinu zilizowapa ushindi

DAR ES SALAAM: KOCHA wa Dodoma Jiji FC, Amani Josiah amesema maandalizi na kuisoma vizuri Mtibwa Sugar FC ndiyo siri ya ushindi wa bao 1-0 walioupata jana katika mchezo wa Ligi Kuu.
Amesema benchi la ufundi la Dodoma Jiji lilifanya uchambuzi wa kina wa mchezo wa Mtibwa Sugar kabla ya kukutana nao na kubaini maeneo yenye udhaifu ambayo waliamua kuyatumia kupata matokeo.
“Tuliwasoma vizuri Mtibwa Sugar, tuliamini katika suala la kumiliki mpira wako na watu wazuri, tukafikiri kuwa tunaweza kucheza kikubwa,” amesema Josiah.
Amesema walibaini baadhi ya maeneo ambayo wapinzani wao walikuwa na mapungufu na wakaamua kuyatumia kwa ufanisi jambo lililowasaidia kupata ushindi huo muhimu.
“Kuna baadhi ya maeneo tuliyabaini kuwa wana mapungufu, tukaamini tukiyatumia vizuri na mojawapo ndiyo hicho kilichofanyika tukapata ushindi wa bao 1-0 jana,” amesema.
Ushindi huo umeifanya Dodoma Jiji kufikisha pointi 28 katika nafasi ya nane ambayo inawasaidia kukimbia kuingia kwenye hatari ya kushuka daraja.



